Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wanaodaiwa kusafirisha nyara za Serikali kusota rumande

Meno Ya Tembo Wanaodaiwa kusafirisha nyara za Serikali kusota rumande

Thu, 13 Jul 2023 Chanzo: mwanachidigital

Upelelezi katika kesi ya kusafirisha meno ya tembo, meno ya simba na kucha za simba inayowakabili watu 12 wakiwemo wafanyakazi wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege (TAA), bado haujakamilika.

Hayo yameelezwa leo Julai 12, 2023 upande wa mashtaka wakati kesi hiyo ya uhujumu uchumi namba 28/2023 ilipoitwa kwa ajili ya kutanjwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Washtakiwa hao wakikabiliwa na mashtaka 11 yakiwemo ya kusafirisha kucha 65 na meno 20 ya Simba, vipande 166 vya meno ya tembo, kughushi vibali vya kusafirisha samaki aina ya Kaa wakiwa hai na kutakatisha fedha kiasi cha Sh3.2 bilioni.

Watuhumiwa hao wanadaiwa kusafirisha nyara hizo kutoka Tanzania, Msumbiji na kuzipeleka Kuala Lumpur, Malaysia bila kuwa na kibali kutoka kwa wakurugenzi wa wanyamapori wa nchini hizo mbili.

Wakili wa Serikali Pancrasia Protas amedai kuwa shauri hilo limeitwa kwa ajili ya kutajwa na upelelezi wake bado unaendelea hivyo ameomba terehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.

Hakimu Mkazi Mkuu anayesikiliza shauri hilo, Rhoda Ngimilanga ameutaka upande wa mashtaka kukamilisha kwa wakati upelelezi, hata hivyo; ameiahirisha kesi hiyo hadi Julai 26, 2023 kwa ajili ya kutajwa.

Kesi hiyo imeendeshwa kwa njia ya video huku washtakiwa hao wakiwa rumande kutokana na mashtaka ya kutakatisha fedha yanayowakabili kutokuwa na dhamana kwa mujibu wa sheria.

Washtakiwa hao ni Abdulah Hamad (58) mfanyabiashara na mkazi wa Ubungo Maziwa, Meneja Mkazi wa Kampuni ya Airline Ltd, Roseline Achachi Wandera (43) mkazi wa Mikocheni; Kennedy Mwambeta na Noel Kasaro ( 41) Mratibu wa Mizigo na mkazi wa Tabata.

Walinzi wawili wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege (TAA), Tito Mwabe (34) na Erasto Makinda (46).

Pia yupo, Theresia Lukanga (40) Wakala wa Mizigo; Abubakari Pazi (32) Wakala wa Mizigo kutoka kampuni ya Smart Ocean.

Washtakiwa wengine ni Haipeng Guo (34) mfanyabiasha na raia wa China; Yassir Husein (50), mfanyabiashara na mkazi wa Arusha pamoja na mfanyabiashara Peter Kikweka (50) mkazi wa Ukonga Mombasa.

Katika mashtaka 11 yanayowakabili washtakiwa hao, mawili ni ya kuongoza genge la uhalifu; matatu ni ya kughushi; matatu mengine ni kutakatisha fedha, wakati mashtaka mawili yanahusu kupatikana na nyara za Serikali, huku shtaka moja kujihusisha na nyara za Serikali.

Miongoni mwa mashtaka hayo ni shtaka la kuongoza genge la uhalifu linalowakabili washtakiwa wote.

Inadaiwa kati ya Januari Mosi 2019 na Mei 27, 2023 katika Uwanja wa Ndege wa Pemba uliopo Mji wa Cabo Delgado Province, uliopo nchini Msumbiji, washtakiwa walipanga genge la uhalifu kwa kupokea, kuuza na kusafirisha vipande 166 vya meno ya tembo.

Vipande hivyo vinatajwa kuwa na thamani ya dola za kimarekani 1,410,000 sawa na Sh 3.285,870,600, mali ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Msumbiji, bila kuwa na kibali kutoka kwa Wakurugenzi wa Wanyamapori.

Chanzo: mwanachidigital