Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wanane kizimbani kwa kusafirisha binadamu

13712 PIC+HUKUMU TanzaniaWeb

Fri, 24 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Watu wanane wamefikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashtaka mawili ya uhujumu uchumi, ikiwemo kuongoza genge la uhalifu na kusaidia kusafirisha binadamu kutoka visiwa vya Comoro kwenda Saudi Arabia kupitia Tanzania.

Washtakiwa hao wamefikishwa mahakamani leo Ijumaa Agosti 24, 2018 mbele ya Hakimu Mkazi, Maira Kasonde na wakili wa serikali Faraji Nguka akishirikiana na Patrick Mwita.

Hata hivyo, washtakiwa Said Ally, Ahmada Mchangama, Hamada Ali na Soulaimana Abdallah hawakusomewa mashtaka yanayowakabili kwa sababu hawafahamu lugha ya Kiingereza wala Kiswahili.

Washtakiwa hao wanne wanafahamu Kiarabu na Kifaransa pekee na mahakama kuamuru wapelekwe rumande hadi Agosti 27, 2018  watakapotafuta mkalimani ili wasomewe mashtaka yanayowakabili.

Kwa upande wa washtakiwa Abdallah Bashrahil, Iddi Said, Muhidin Machelenga na Swed Swed wao walisomewa mashtaka hayo mahakamani hapo.

Akiwasomea mashtaka hayo katika kesi hiyo ya uhujumu uchumi namba 64 ya mwaka 2018, wakili wa Serikali, Faraja Nguka amedai washtakiwa hao waliongoza genge la uhalifu katika maeneo tofauti kati ya Tanzania na Comoro.

Washtakiwa hao wanadaiwa kusafirisha binadamu kutoka Comoro kwenda Saudi Arabia kupitia Tanzania.

Nguka katika shtaka la pili amedai kuwa washtakiwa hao wanadaiwa kusaidia usafirishaji wa binadamu.

Washtakiwa hao wanadaiwa kuwa katika sehemu tofauti jijini Dar es Salaam, Tanzania na Comoro waliwasafirisha Halima Mmadi mwenye hati ya kusafiria namba NBE 337205, Tereha Mlahaili (NBE 45463) na  Ali Miraaji (NBE 415463) na watu wengine 162.

Imedaiwa kuwa washtakiwa hao walifanya urahisi wa kuwasafirisha watu hao kwa kuwapatia hati za kusafiria za Tanzania wakati wakijua ni raia wa Comoro.

Baada ya kusomewa mashtaka hayo, washtakiwa hao hawakuruhusiwa kuongea chochote kwa sababu mahakama hiyo haina mamlaka ya kuisikiliza kesi hiyo hadi Mahakama Kuu kitengo cha rushwa.

Upande wa mashtaka umedai upelelezi bado haujakamilika na kesi hiyo kuahirishwa hadi Agosti 27, 2018 itakapotajwa tena.

Washtakiwa wanatetewa na mawakili Jeremiah Mtobesya na Nehemiah Nkoko.

Washtakiwa walipelekwa rumande kwa sababu mashtaka ya kusafirisha binadamu ni miongoni kwa mashtaka yasiyo na dhamana.

Chanzo: mwananchi.co.tz