Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wanandoa, maofisa TRA kizimbani dawa za kulevya

70cffb2ea8607a72daa244503bdf9aff.jpeg Wanandoa, maofisa TRA kizimbani dawa za kulevya

Tue, 20 Jul 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

MAMLAKA ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini (DCEA) kwa kushirikiana na vyombo vingine vya usalama wamekamata dawa za kulevya kilo 99.3 mwezi uliopita katika matukio tofauti mkoani Dar es Salaam.

Kamishna Jenerali wa DCEA, Gerald Kusaya jana aliwaeleza waandishi wa habari jana Dar es Salaam kuwa watu wanane walikamatwa wakiwemo watumishi watatu wa serikali.

Kusaya alisema Dar es Salaam kuwa watuhumiwa wote wamefikishwa mahakamani wakikabiliwa na makosa ya kujihusisha na usafirishaji wa biashara ya dawa za kulevya.

“Mtakumbuka kua Juni 16, 2021 nilitoa taarifa juu ya kukamatwa kwa kilo 88.33 za dawa za kulevya zikiwa ndani ya gari aina ya Toyota Prado namba T503 DHC ikiwa imetelekezwa barabarani katika eneo la Kimara Korogwe, Dar es Salaam na nikawaambia tunaendelea na uchunguzi wa tukio hilo,” alisema Kusaya.

Aliongeza, “Katika uchunguzi wetu tulibaini kuwa kati ya kilo 88.27 zilizokamatwa wakati ule, kuna dawa nyingine ziliibiwa na baadhi ya watumishi wasio waamini walishiriki katika uhalifu huo.”

Kusaya alisema Juni 21, mwaka huu Mivinjeni Wilaya ya Temeke walimkamata ofisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Andrew Paul (45), mkazi wa Kurasini.

“Mtuhumiwa huyo alikamatwa na wenzake Said Mgoha (45) maarufu kama Kindimu kazi yake fundi gereji mkazi wa Mtoni Kijichi, na George Mwakang’ata (38) mfanyabiashara na mkazi wa Mtoni Kijichi wakiwa na dawa za kulevya aina ya heroin kiasi cha kilo 1.02,” alisema Kamishna Jenerali Kusaya.

Aliwataja washitakiwa wengine kuwa ni Ally Juma (32) ofisa wa TRA ambaye alikamatwa Juni 23, mwaka huu.

“Alikamatwa pamoja na Abubakar Abdalla (28) mfanyabiashara wakiwa na dawa za kulevya aina ya methamphetamine zenye uzito wa gramu 597.61, katika upekuzi uliofanyika nyumbani kwa Ally maeneo ya Zimbili Kinyerezi kulipatikana pesa taslimu Sh 82,043,000 na USD (Dola za Marekani) 5,100,” alisema Kusaya.

Katika tukio lingine Juni 19, Bunju Beach walimkamata aliyekuwa askari polisi F 6763 Koplo Deodatus Massare (37) akiwa na kilo 1.04 za dawa za kulevya aina ya heroin.

“Katika tukio lingine mnamo Juni 18, 2021 katika eneo la Mburahati Madoto NHC tulifanikiwa kuwakamata mume na mke ambao ni Jamal Nangatukile (45) na Mariyam Bacha (28) wakiwa na dawa za kulevya aina ya heroin yenye uzito wa gramu 494.52,” alisema Kusaya.

Alisema wanaendelea kuchunguza kuwabaini wahalifu wengine walioshiriki katika matukio hayo na akaonya wanaotaka kujaribu makali ya serikali kwa kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya.

“Pia niwaombe waandishi kuendelea kutumia kalamu yao kuwapa elimu Watanzania kuhusu madhara ya biashara hiyo na matumizi ya dawa za kulevya kwa tusiposhughulikia janga hilo tutaua nguvu kazi ya taifa letu,” alisema Kusaya.

Chanzo: www.habarileo.co.tz