Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wananchi waishi kwa hofu kuuawa Masasi

DC Masasi Wananchi waishi kwa hofu kuuawa Masasi

Wed, 17 Aug 2022 Chanzo: Mwananchi

Wananchi wa Kata ya Nyasa, Wilaya ya Masasi mkoani Mtwara, wamesema wamekuwa wakiishi kwa hofu baada ya wanawake watatu kuuawa katika kata yao.

Hofu hiyo imeibuliwa na Joyce Wajetu, mkazi wa kata hiyo mbele ya Mkuu wa Wilaya ya Masasi, Cloudia Kitta aliyefika kuzungumza na wananchi wa eneo hilo.

Joyce alisema kumekuwa na ngoma aina ya vigodoro zisizoisha na pombe zinazouzwa kuanzia asubuhi,a hali aliyosema inaweza kuwa chanzo cha kuwapo kwa matukio ya ukatili yanayosababisha mauaji kwa wanawake.

“Mfano yule mama alipouawa alikuwa anauza vyombo, masikini tena vyombo vya plastik akauawa na bado waliomuua wametolewa. Hii inawafanya wauaji waendelee kufanya matukio ya ajabu, kwa nini hatuoni wahalifu wakichukuliwa hatua?” alihoji Joyce

Wiki iliyopita, Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara, Nicodemus Katembo alizungumzia matukio hayo akiwataja miongoni mwa waliouawa ni Mwanahawa Hashimu, mwalimu wa Shule ya Msingi Mbaju ambaye alifariki akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa Ndanda.

Mwingine ni Fatma Bakari, aliyeuawa na watu wasiojulikana baada ya kulawitiwa ndani ya gofu jirani na nyumbani kwao.

Advertisement Alisema mwili ulifanyiwa uchuguzi na kubaini chanzo cha kifo chake ni kukosa hewa, baada ya uso kugandamizwa ardhini kwa muda mrefu.

Akizungumza katika mkutano huo, Kaimu Sheikh wa Wilaya ya Masasi, Hashimu Anafi alisema ulevi umekuwa mkubwa katika eneo hilo, na kwamba vijana muda wote wanavuta bangi na kulewa, hivyo lazima matukio hayo yakemewe ili kulinda familia.

“Madhara ya uvutaji wa bangi, ulevi uliokithiri, mtu anaelewa kutwa nzima wakati hana hata mia, ndio maana wakiona mtu anapita wako tayari kumbaka ili wapate hela ya kulewa. Mtu yuko tayari kuua, kuumiza mtu ili apate pesa ya kunywa pombe,” alisema.

Naye Kitta alikemea vitendo vya mauaji ya wanawake vilivyotokea wilayani humo, huku akiwataka wanaofanya vitendo hivyo kuacha mara moja.

‘‘Matukio haya hayakubaliki kwa kuwa ni kinyume na sheria za nchi na dini. Pia tunapaswa kukemea matukio ya mauaji kama haya ya wanawake,’’ alisema.

“Najua mmeguswa na hali hii ili isiendelee tena tuimarishe ulinzi shirikishi ambapo Polisi kata atakuja na kuungana na wananchi ili kuimarisha na kuboresha ulinzi shirikishi. Jeshi letu lina maofisa wachache, hivyo lazima tuungane nao ili tuweze kufanikisha ulinzi kwenye mitaa na kunusuru hali hii,” alisema Kitta.

Chanzo: Mwananchi