Dar es Salaam. Raia watatu wa Nigeria akiwemo mchungaji wameandika barua kwa mkurugenzi wa mashtaka nchini Tanzania (DPP) kukiri kosa la uhujumu uchumi linalowakabili.
Washtakiwa hao, Henry Ozoemana Ogwuanyi (mchungaji), Onyebuchi Ogbu na Lucy Oding
wanakabiliwa na kesi ya kukutwa na kilo 15.8 za dawa za kulevya aina ya Heroin.
Wakili wa Serikali, Elia Athanas ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu leo Alhamisi Oktoba 24, 2019 kuwa washtakiwa hao wameandika barua kwa DPP kwa ajili ya kuomba msamaha na kukiri makosa yanayowakabili.
"Washtakiwa wameandika barua ya kukiri makosa yao lakini DPP bado hajajibu barua hiyo, naiomba mahakama ipange tarehe nyingine,” amedai Athanas.
Baada ya maelezo hayo wakili wa utetezi, Hassan Kiangio amedai suala la kuandika barua kwa washtakiwa hao isiwe kikwazo cha kutoendelea na kesi hiyo, kuuomba upande wa mashtaka kukamilisha upelelezi ili shauri hilo liende mbele.
Habari zinazohusiana na hii
Hakimu Shaidi ameahirisha shauri hilo hadi Novemba 6, 2019 itakapotajwa.Katika kesi ya msingi inadaiwa Aprili 21, 2019 eneo la Msimbazi wilaya ya Ilala jijini Dar es Salaam washtakiwa walikutwa na dawa za kulevya aina ya Heroin kilo 15.8.