Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wamwagiwa mchanga wakisoma darasani

E3d44c92002bca068431d949ddf04b58 Wamwagiwa mchanga wakisoma darasani

Tue, 27 Oct 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

NAIBU Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana na Ajira, Anthony Mavunde amesema mpango wa serikali ni kuona majengo yake ya shule yanafanyiwa ukarabati ili kuondoa changamoto za miundombinu.

Aidha amesema serikali kwa kushirikiana na wadau wa elimu itahakikisha inawaondolea wanafunzi kero ya kumwagiwa mchanga na kukosekana kwa usikivu wanapokuwa madarasani.

Alisema hayo wakati akijibu risala aliyosomewa na wanafunzi wa shule ya msingi Makole jijini hapa kwenye mahafali ya darasa la saba yaliyofanyika shuleni hapo.

Wanafunzi hao walisema changamoto waliyonayo kwenye shule hiyo ni kuwepo kwa mwingiliano wa watu ambao mara nyingi wamekuwa wakipita karibu na madirisha na kusababisha kukosa usikivu wakati wanapokuwa madarasani kwa sababu ya shule kutokuwa na uzio.

Leah Herman akisoma risala hiyo kwa niaba ya wanafunzi hao, alisema changamoto nyingine ni kumwagiwa mchanga madirishani na kupigiwa kelele na vijana wanaopita karibu na madirisha na kusababisha hofu na usalama wao pamoja na walimu wanaowafundisha.

Alisema changamoto hiyo inaweza kutatuliwa na serikali kwa kushirikiana na jamii kama wataweza kuwekeza michango yao ya mali na fedha ili kukarabati miundombinu hiyo ambayo inayohitaji.

Kwa upande wake Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Veronica Mrope alisema changamoto waliyonayo inatokana na kuwa na mwingiliano wa watu ambao mara kwa mara wamekuwa wakipita bila kujali kuwa wanafunzi hao wanajisomea na wanahitaji utulivu.

"Tatizo shule yetu ipo barabarani, wengi wanaopita hapa ikiwemo magari, waendesha bodaboda na wapita kwa miguu, lakini kibaya zaidi kuna baadhi ya vijana wamefikia hatua hata ya kuwamwagia mchanga wanafunzi wanapokuwa madarasani, hii yote ni kwa sababu hatuna uzio ambao unaoweza kuzuia," alisema.

Shule hiyo ambayo ina wanafunzi 1,100 alisema kutokana na hali ya kukosa uzio wanaiomba serikali pamoja na wazazi na jamii kujitoa kwa hali na mali ili kufanikisha uhitaji huo wa kuwepo kwa uzio ambao utaweza kusaidia kuondokana na kero wanayokutana nayo wanafunzi na walimu hivi sasa.

Chanzo: habarileo.co.tz