Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wambura aendelea kusota rumande

Thu, 23 May 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Aliyekuwa Makamu wa Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Michael Wambura anayekabiliwa na kesi ya utakatishaji fedha anaendelea kusota rumande kutokana na upelelezi wa shauri hilo kutokamilika.

Wakili wa Serikali, Fatma Waziri amedai hayo leo Alhamisi Mei 23, 2019 katika mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mbele ya Hakimu Mfawidhi,  Kelvin Mhina, akibainisha kuwa kesi hiyo imekuja kwa ajili ya kutajwa na upelelezi bado unaendelea.

Hakimu Mhina ameahirisha  kesi hiyo hadi Juni 4, 2019 itakapotajwa tena huku Wambura akirudishwa rumande  kutokana na mashtaka yanayomkabili kutokuwa na dhamana.

Wambura alifikishwa Kisutu kwa mara ya kwanza, Februari 11, 2019  akikabiliwa na mashtaka 17 yakiwemo ya kutakatisha fedha zaidi ya Sh100 milioni katika kesi ya uhujumu uchumi namba 10/2019.

Katika mashtaka hayo 17, moja ni la kughushi, shtaka moja la kutoa na kuwasilisha nyaraka za uongo,  mashtaka 13 ya kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na mashtaka mawili ya kutakatisha fedha haramu.

Katika kesi ya msingi inadaiwa kuwa Juni 6, 2004 sehemu isiyojulikana ndani ya Jiji la Dar es salaam mshtakiwa anadaiwa kutenda kosa la kughushi.

Pia Soma

Siku hiyo, Wambura kwa nia ya kutapeli alitengeneza barua ya  kughushi ambayo haina kumbukumbu namba akionyesha imeandikwa na E Maganga ambaye ni mtendaji Mkuu wa  kampuni ya Jeck System anadai kurejeshewa malipo ya mkopo wa Dola 30,000 za Marekani pamoja na riba aliyokuwa ameikopesha TFF.

Katika shtaka jingine,  Wambura anadaiwa kutoa na kuwasilisha nyaraka ya uongo, iliyokuwa haina kumbukumbu namba  ya Julai 6, 2004, akijifanya kwamba ni barua iliyoandikwa na E. Maganga ambaye ni mtendaji Mkuu wa Jeck System Ltd, akionyesha kuwa anadai mkopo wa Dola 30,000 za Marekani pamoja na riba waliokopeshwa TFF huku akijua kuwa sio kweli.

Hata hivyo, kuanzia  shtaka la tatu hadi la 15 mshtakiwa anadaiwa kujipatia kiasi cha zaidi Sh95 milioni, kwa njia ya udanganyifu akidai kuwa fedha hizo ni sehemu ya malipo ya jumla ya kiasi cha fedha mbalimbali na riba kutoka kwa kampuni ya Jeck System Ltd huku akijua kuwa siyo kweli.

Katika mashtaka ya kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu, Wambura anadaiwa kutenda kosa hilo Juni 17, 2015 huko katika ofisi za TFF ambapo kwa njia ya udanganyifu, mshtakiwa alijipatia Sh10milioni kutoka TFF kwa kuonyesha kuwa ni malipo ya Dola 30,000 za Marekani pamoja na riba kutoka kwenye kampuni hiyo ya Jeck jambo ambalo sio kweli.

Katika shtaka la utakatishaji fedha, Wambura anadaiwa  kati ya Agosti 15 na Oktoba 21, 2014, makao makuu ya Shirikisho hilo,  alijipatia Sh25milioni  kutoka TFF huku akijua fedha hizo ni zao la kosa la kughushi.

Pia, shtaka jingine utakatishaji fedha haramu, mshtakiwa anadaiwa kati ya Machi 16 na Oktoba 21,  2015 alijipatia Sh75,947,924 kutoka TFF wakati akijua fedha hizo sio halali na zimetokana na shtaka la kughushi.

 

Chanzo: mwananchi.co.tz