Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Waliovunja ofisi na kuiba pikipiki wafungwa miaka sita

HUKUMU Waliovunja ofisi na kuiba pikipiki wafungwa miaka sita

Tue, 19 Sep 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Watu wawili akiwemo raia wa Burundi, Niyokindi Anthony (44), wamehukumiwa kutumikia kifungo cha miaka sita jela baada ya kukiri kutenda kosa la kuvunja Ofisi ya Mganga Mkuu (DMO) wilaya ya Sengerema mkoani Mwanza na kuiba pikipiki tatu zenye thamani ya Sh11, 850,000.

Mshtakiwa mwingine aliyehukumiwa kutumikia kifungo hicho ni mkazi wa Isungangh'olo wilayani Sengerema mkoani humo, Ibrahim Mshengezi (55) ambapo wamehukumiwa kwa kutenda makosa mawili ambayo ni kuvunja Ofisi na kuiba kinyume na vifungu 297 na 258 vya Kanuni ya Adhabu sura ya 16 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2022.

Katika kesi hiyo yenye washtakiwa watatu, mshtakiwa mwingine ambaye ni Mkazi wa Isungangh'olo wilayani Sengerema, Anold Paul (25) amekana mashtaka hayo ambapo Hakimu Mkazi Mwandamizi wa Mahakama hiyo, Evod Kisoka ameamuru arejeshwe rumande baada ya kukosa wadhamini.

Awali, akiwasomea maelezo ya kosa washtakiwa, Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Sajenti wa Polisi Theophilius Bei amesema washtakiwa walitenda makosa hayo Agosti 20,2023, kwa kuiba pikipiki tatu za Serikali zenye namba ya usajili, SM15342, SM15343 na SM15349, zote kampuni ya Yamaha kinyume na Kanuni ya adhabu Sura ya 16 toleo la mwaka 2022.

Hata hivyo, shtaka dhidi ya mshtakiwa namba tatu (Anold Paul) ambaye amekana mashtaka hayo litaendelea tarehe 2/10/2023.

Hakimu Kisoka amesema mahakama inatoa hukumu ya miaka sita kwa washtakiwa ili iwe funzo kwa wengine.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live