Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Waliounganisha maji kiholela watakiwa kujisalimisha

10616 Pic+dawasco TanzaniaWeb

Tue, 7 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Shirika la Majisafi na Majitaka Dar es Salaam (Dawasco) limeanza kutekeleza agizo la Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Profesa Makame Mbarawa la kuwataka wananchi waliojiunganishia maji kinyemela kujisalimisha.

Julai 30, 2018 Waziri Mbarawa alitoa miezi miwili kwa wateja hao kujisalimisha Dawasco ili waunganishwe katika mfumo rasmi bure la sivyo hatua kali za kisheria zitachukuliwa.

Taarifa kwa umma iliyotolewa leo Agosti 7, 2018 na ofisi ya uhusiano ya Dawasco imeeleza agizo la Waziri Mbarawa limeanza kutekelezwa kuanzia Agosti hadi Oktoba, 2018.

Dawasco imewataka wakazi wa Dar es Salaam, Mji wa Bagamoyo na Kibaha mkoani Pwani wafike ofisi za shirika hilo kwa ajili ya kuunganishwa katika mfumo rasmi.

"Wananchi ambao wamejiunganishia huduma ya maji bila kibali, shirika linawataka kufika katika ofisi yoyote ya Dawasco iliyo karibu kwa ajili ya kusajiliwa na usajili utafanyika bure bila faini yoyote kwa kipindi hiki."imesema taarifa hiyo.

"Baada ya kazi ya usajili kukamilika, kutakuwa na msako mkali wa nyumba kwa nyumba na wananchi watakaobainika watachukuliwa hatua kali za kisheria ikiwamo kufikishwa mahakamani kwa kosa la uhujumu uchumi, " imeeleza taarifa hiyo.

Chanzo: mwananchi.co.tz