Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Waliotozwa faini ya magari wakakwepa, kiama kimeanza leo

35355 Pic+ubungo Waliotozwa faini ya magari wakakwepa, kiama kimeanza leo

Wed, 9 Jan 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani wameanza operesheni ya kukagua magari yote yaliyoandikiwa faini lakini hayajalipa ndani ya siku saba kwa mujibu wa sheria.

Operesheni ya ukaguzi huo imeanza leo, Jumanne Januari 8, 2018 katika maeneo mbalimbali nchini na kwa upande wa Dar es Salaam imefanyika kwenye kituo cha mabasi Ubungo.

Ofisa Operesheni wa Trafiki makao makuu, Kamanda Abdi Issango amesema ukaguzi huo utayahusu magari yote yakiwamo mabasi yanayokwenda mikoa mbalimbali ambayo yaliandikiwa faini lakini hayajalipa.

“Mfumo huu wa mashine za kieletroniki ukiandikiwa faini ya 30,000 unatakiwa uilipe ndani ya siku saba. Lakini ikifika siku ya nane hukulipa itakupasa ulipe Sh 37,500 ambayo tunaliita ndio deni baada ya muda kupita ,”amesema Kamanda Issango.

Kwa mujibu wa Kamanda Issango, wamebaini yapo magari mengi yakiwamo ya mkoani yameandikiwa faini kutokana na makosa mbalimbali lakini bado hawajazilipa na muda umeshapitiliza.

Amesema ukaguzi uliofanyika kwa mabasi 90 ya mikoani kati ya 31 yamebainika kuwa na madeni na wahusika wake wamelazimika kuyalipa papo hapo na zaidia ya Sh3milioni zilizipatikana.

Kamanda Issango amesema ukaguzi huo utafanyika maeneo mbalimbali lakini kwa mabasi ya mikoani utakuwa ni stendi kabla ya kuanza safari zake na tayari ameshatoa maelekezo kwa wakuu wa usalama wa barabarani wa mikoani.

Katika hatua nyingine, Kamanda Issango aliamuru basi la kampuni la Tashrif  linalofanya safari zake Tanga na Dar es Salaam, kulipa faini baada ya baadhi ya siti kubainika hazina mikanda kwa ajili ya abiria jambo ambalo linaweza kuhatarisha usalama wa abiria hao.

Akizungumzia faini hiyo, dereva wa basi hilo Abdallah Yusuf amesema: “Najutia kosa hili, na hii inatokana na kukosa muda wa kuifunga kutokana na abiria kuwa wengi ambao wanataka kusafiri. Naahidi tutalishughulikia tatizo hili muda si mrefu,” amesema Yusuf.



Chanzo: mwananchi.co.tz