Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Walioshitqkiwa kwa kusafirisha kilo 164 za mirungi washinda kesi

Vijiji Vitatu Vyaacha Kulima Mirungi Same.png Walioshitqkiwa kwa kusafirisha kilo 164 za mirungi washinda kesi

Tue, 19 Dec 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imewaachia huru wafanyabiashara watatu waliokuwa wanakabiliwa na shtaka moja la kusafirisha dawa za kulevya aina ya mirungi, baada ya Serikali kushindwa kuthibitisha shtaka dhidi yao.

Walioachiwa huru ni Ahmed Ally (42) mkazi wa Kigamboni, Mohamed Mbegu (35) mkazi wa Ukonga na Ramadhani Mkude (42), mkazi wa Kitunda.

Washtakiwa hao kwa pamoja walikuwa wanakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi namba mbili ya mwaka 2022.

Katika kesi hiyo, washtakiwa hao walikuwa wanadaiwa kusafirisha kilo 164.39 za Mirungi, kinyume cha sheria.

Uamuzi huo umetolewa leo, Desemba 18, 2023 na hakimu Mkazi Mkuu, ushindi Swalo, wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya kutolewa hukumu.

Hakimu Swalo alisema upande wa mashtaka ulipeleka mashahidi 12 kwa ajili ya kuthibitisha shtaka linalowakabili washtakiwa hao.

Akipitia ushahidi huo, alisema ushahidi uliotolewa na askari waliokamata vielelezo hivyo (mirungi) waliieleza Mahakama kuwa Mirungi hiyo ilikuwa katika mifuko ya kaki.

Lakini maelezo ya shahidi huru aliyeshuhudia ufungaji wa vielelezo hivyo, yanatofautia na maelezo ya askari Polisi walihusika katika ukamataji.

Hakimu Swalo alisema shahidi huru alieleza Mahakama kuwa Mirungi hiyo ilivyokamatwa ilikuwa haijafunikwa na kitu chochote, bali ilikuwa imefungwa kamba huku ikiwa na majani yake.

Pia shahidi aliyeshuhudia wakati wa ukamataji alisema Mirungi hiyo ilikuwa wazi na wala haikuwa imefunikwa kwenye mfuko wa kaki.

Hakimu Swalo, pia alisema wale mashahidi waliobeba vielelezo( Mirungi) kutoka Chanika kuvileta Kituo Kikuu Cha Polisi( Central), hawakuja mahakamani kutoa ushahidi.

Akiendelea kuchambua ushahidi wa upande wa mashtaka, Hakimu Swalo alisema hata maelezo ya onyo ya washtakiwa yaliyochukuliwa Kituo Kikuu cha Polisi( Central) Dar es Salaam, yalitofautia kwani kuna shahidi alieleza kuwa washtakiwa walifikishwa kituoni hapo Desemba 28, 2021, saa 11:45 jioni na baadae walipelekwa Kitengo cha Kuzuia na Kupambana ba Dawa za Kulevya( ADO) kilichopo chini ya Jeshi la Polisi,  kwa ajili ya kuandikwa maelezo.

Lakini askari polisi aliyekuwa zamu siku hiyo katika Kituo Kikuu cha Polisi, ambaye ndiyo aliyewapokea washtakiwa hao alidai kuwa washtakiwa baada ya kufikishwa Central hawakutoka siku hiyo.

"Kwa maelezo hayo, Mahakama inaona kuwa yanaleta shaka na baadhi ya mashahidi wanatoafautiana katika ushahidi wake wao. " alisema Hakimu Swalo na kuongeza

"Hivyo, baada ya kupitia ushahidi wa mashahidi 12 uliotolewa na upande wa mashtaka, Mahakama imeona upande wa mashtaka wameshindwa kudhibitisha kesi hii bila kuacha mashaka, inawaachia huru washtakiwa hawa " alisema hakimu Swalo.

Awali, wakili wa Serikali Happy Mwakanyamale alidai kuwa kesi hiyo iliitwa kwa ajili ya kutolewa hukumu na upande wa mashtaka upo tayari.

Kwa mara ya kwanza, washtakiwa hao walifikishwa mahakamani hapo Januari 6, 2022.

Hata hivyo, kesi hiyo ilianza kusikilizwa Novemba 23, 2023 ambapo upande wa mashtaka walipeleka mahakamani mashahidi 12.

Washtakiwa hao ambao walikuwa wanatetewa na wakili Constantine Kakula, walikutwa na kesi ya kujibu Desemba 5, 2023.

Katika utetezi wao ambao walijitetea kwa njia ya kiapo, walidai kuwa tuhuma zinazowakabili sio za kweli, hivyo wanaiomba Mahakama iwaone hawana hatia na kuwaachia huru.

Washtakiwa baada ya kumaliza kujitetea, mahakama ilifanya majumuisho ya kesi kabla ya kutoa hukumu.

Katika kesi ya msingi, washtakiwa hao wanadaiwa Desemba 29, 2021 katika eneo la Nyeburu lililopo Chanika, wilaya ya Ilala.

Washtakiwa hao wanadaiwa siku hiyo ya tukio majira ya usiku, walikutwa wakisafirisha Mirungi yenye uzito wa kilo 164.39 kwa kutumia usafiri wa bodaboda.

Inadaiwa siku hiyo usiku, Askari Polisi waliokuwa doria eneo hilo, walipewa  taarifa kutoka mwa msiri kuwa kuna watu wanauza Mirungi eneo la Nyeburu.

Askari baada ya kupata taarifa hiyo, walienda eneo la tukio na kukuta pikipiki mbili zikiwa zimebeba mirungi.

Baada ya kuwakamata watu hao, walipelekwa Kituo Kikuu cha Polisi (Central) Dar es Salaam kwa ajili ya hatua nyingine.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live