Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Waliomuua na kumtoa kizazi mtoto wahukumiwa kunyongwa

Wanyongwa Picrd Waliomuua na kumtoa kizazi mtoto wahukumiwa kunyongwa

Mon, 3 Apr 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Watu wawili, akiwemo mganga wa kienyeji, Mbwana Makamba, wamehukumiwa kunyongwa hadi kufa baada ya kukutwa na hatia ya kumuua mtoto, Samira Said (4), kisha kumtoa kizazi na kuondoka nacho.

Waliohukumiwa adhabu hiyo ni Richard Kimweri (43) ambaye alikuwa mlinzi na mkazi wa eneo la Makaburi ya Baniani na Mbwana Makamba ambaye ni mganga wa kienyeji na mkazi wa Daraja II.

Hukumu hiyo iliyotolewa juzi na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, Joachim Tiganga ambaye alieleza Mahakama imewatia hatiani watuhumiwa hao baada ya kukutwa kwa kosa la mauaji kinyume na vifungu vya 196 na 197 vya Kanuni ya Adhabu na kuwahukumu kunyongwa hadi kufa.

Alieleza ushahidi wa jamhuri umethibitisha watuhumiwa hao walitenda kosa hilo ambapo miongoni mwa mambo Mahakama iliyoyazingatia ni mshtakiwa wa kwanza (Kimweri) kukiri kupitia maelezo yake ya onyo ambapo pia alimtaja mshtakiwa wa pili.

Aidha nguo za marehemu, ikiwemo suruali zilizokutwa nyumbani kwa mshtakiwa wa kwanza zilitambuliwa na wazazi wa marehemu.

Jaji Tiganga alitaja ushahidi mwingine ambao ulikuwa muhimu uliowaunganisha washtakiwa hao moja kwa moja na kuhusika kwa kosa hilo ni ripoti ya uchunguzi wa vinasaba (DNA), ambavyo vilichukuliwa kutoka kwenye uke wa mtoto huyo na sampuli zilizochukuliwa kwenye kucha na mikono ya washtakiwa hao zilikuwa zinafanana.

Kupitia mashahidi wa jamhuri ilielezwa mahakamani hapo kuwa siku ya tukio mtoto huyo akiwa anacheza na watoto wenzake, mshtakiwa wa kwanza alimfuata na kumdanganya atamnunulia pipi amfuate, ambapo aliondoka naye na mtoto huyo hakuonekana tena.

Alikuja kukutwa amefariki majira ya saa tatu usiku, ambapo ilidaiwa baada ya kumchukua marehemu walienda naye nyumbani kwa mshtakiwa wa kwanza. Aidha kupitia maelezo ya onyo ya Kimweri, alikiri kuwa alipofika nyumbani kwake mganga huyo aliingiza mkono kwenye uke wa marehemu na kumtoa kizazi ambapo alishafariki kabla ya kutoa kizazi hicho na walisubiri giza liingie kisha wakaenda kumtupa barabarani.

Ilielezwa Juni 22, 2016 wakati wa upekuzi nyumbani kwa Richard zilikutwa baadhi ya nguo za mtoto huyo pamoja na suruali ya mshtakiwa ikiwa na damu, ambapo alikiri kushirikiana na Makamba ambaye alikuwa mganga wa kienyeji aliyemtaka atafute kizazi cha mtoto ili apate utajiri.

Kwa upande wake Makamba katika maelezo yake ya onyo alikiri kumwingizia marehemu mkono na kumtoa kizazi.

Maelezo yaliyoungwa mkono na maelezo ya daktari ambaye aliieleza Mahakama sehemu za siri za mtoto huyo zilikuwa zimeharibika.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live