Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Waliomteka mwanamke Dar, walipa faini, fidia, mmoja agoma kukiri mashtaka

HUKUMU Waliomteka mwanamke Dar, walipa faini, fidia, mmoja agoma kukiri mashtaka

Thu, 7 Mar 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Washtakiwa sita wamelipa faini ya Sh 300,000 kila mmoja baada ya kupatikana na hatia ya kumteka mwanamke na kisha kumshikilia kwa siku nne mfululizo.

Hukumu hiyo ilitolewa jana na Hakimu Mkazi Mkuu, Aaron Lyamuya wa Mahakama ya Kisutu, Dar es Salaam, hivyo washtakiwa hao kuepuka kwenda jela miaka mitatu.

Hukumu hiyo imetolewa baada ya washtakiwa hao kuingia makubaliano na Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) ya kukiri kosa.

Washtakiwa hao ni Assad Abdulrasur (43), mkazi wa Msasani Village, Fahad Mussa(33) mkazi wa Dodoma Airport, Nathan Jothan(27), mkazi wa Sinza na Nicolas Nilahi (39), mkazi wa Wazo Hill. Wengine ni Fredy Chahoza (49) mkazi wa Chamwino Dodoma; Ifan Saleh (41) mkazi wa Kisemvule.

Walishtakiwa kwa kosa la kumteka Han Nooh Husein, Oktoba 16, 2023 eneo la Msasani Beach, wilaya Kinondoni.

Pamoja na adhabu hiyo, pia Mahakama imeamuru kila mshtakiwa kumlipa mlalamikaji (Han) fidia ya Sh500,000 kwa kumsababishia maumivu na mateso.

Hata hivyo, mshtakiwa wa saba, Hassan Nur (39) mkazi wa Msasani Village A, hakufanya majadiliano na DPP ya kukiri mashtaka hayo, hivyo kesi yake itaendelea kusikilizwa Machi 20, 2024.

Akisoma uamuzi huo, Hakimu Lyamuya amesema Mahakama imewatia hatiani washtakiwa hao kupitia makubaliano waliyofanya na DPP.

"Washtakiwa sita, nawatia hatiani kwa kosa mlilokiri la kuteka kupitia makubaliano mliofanya na DPP,” amesema Hakimu Lyamuya.

Kabla ya kutolewa kwa adhabu hiyo, wakili wa Serikali Frank Michael alidai kesi hiyo iliitwa kwa ajili ya uamuzi baada ya washtakiwa sita kati ya saba kufanya majadiliano na DPP ya kuimaliza kesi yao kwa njia ya makubaliano.

Amesema washtakiwa hao walikuwa wanakabiliwa na mashtaka mawili ambayo ni unyang'anyi wa kutumia silaha na kuteka.

Hata hivyo, baada majadiliano na DPP Februari 29, 2024, wakafutiwa shtaka la unyang'anyi na kubaki na shtaka moja la kuteka lililowatia hatiani.

Alidai kutokana na mahakama kuwatia hatiani washtakiwa hao, aliiomba mahakama itoe adhabu kulingana na mapendekezo waliyokubaliana katika mkataba waliongia baina ya washtakiwa na DPP.

“Mheshimiwa hakimu, upande wa mashtaka hauna kumbukumbu za makosa ya nyuma dhidi ya washtakiwa hawa, hivyo tunapendekeza adhabu tuliyokubaliana katika mkataba baina ya washtakiwa na DPP ambayo ni kifungo cha miaka mitatu jela na adhabu nyingine ambazo mahakama itaona zinafaa" aliiambia Mahakama.

Washtakiwa wajitetea

Baada ya kutiwa hatiani kwa kosa hilo, Mahakama ilitoa nafasi kwa washtakiwa kujitetea na kupitia jopo la mawakili wanne wa utetezi likiongozwa na wakili Hekima Mwasipu akishirikiana na William Fungo, Mkadamu Mkadamu na Steven Byabato, uliomba mahakama itoe adhabu ndogo yenye unafuu kwa wateja wao kwa kuwa hawajaisumbua Mahakama.

Mwasipu alidai washtakiwa wote waliingia makubaliano ya kukiri mashtaka kwa ridhaa yao.

“Washtakiwa hawa wanategemewa na wazazi wao, familia zao, wake zao na watoto na pia mshtakiwa wa tatu (Nathan) mke wake ni mjamzito anatarajia kujifungua muda wowote kuanzia sasa, mheshimiwa hakimu tunaomba mahakama yako itoa adhabu nafuu,” aliomba Mwasipu.

Akitoa adhabu

Baada ya maelezo hayo, Hakimu Lyamuya amesema Mahakama imezingatia shufaa za pande zote na pia imezingatia makubaliano ya walioingia washtakiwa na DPP na kwamba anaamini washtakiwa kukaa rumande kwa miezi minne wamejifunza.

“Hivyo, kwa kuzingatia mazingira yenyewe yaliyotendeka kosa, kumteka mtu kwa siku nne na kwa kuzingatia shufaa za washtakiwa walizozitoa hapa mahakamani kupitia mawakili wao, Mahakama inawahukumu kila mmoja kulipa faini ya Sh300,000 au kwenda jela miaka mitatu,” amesema Hakimu Lyamuya na kuongeza;

“Pia mahakaka hii inawaamuru kila mshtakiwa kumlipa mlalamikaji fidia ya Sh500,000 kutokana na kumsababishia maumivu na mateso baada ya kumteka na kumshikilia kwa siku nne mfululizo.”

Hata hivyo, Hakimu Lyamuya amesema washtakiwa wana haki ya kukata rufaa kupinga adhabu waliyopewa na si kupinga kutiwa hatiani.

Kesi ya msingi

Katika kesi ya msingi, washtakiwa kwa pamoja wanadaiwa kumteka Han Hussein Oktoba 16, 2023 eneo la Beach ya Msasa, lililopo wilaya Kinondoni.

Inadaiwa, siku hiyo, washtakiwa walitumia nguvu na kumteka Han, aende mtaa wa Ujirani uliopo Mbezi Beach na alipofika hapo, walimchukua na kumpeleka katika nyumba ya Haidary Waziri na kisha kushikilia kwa simu nne, wakati wakijua ni kinyume cha sheria.

Novemba 7, 2023, Serikali iliwasomewa washtakiwa hao maelezo ya awali ( PH) na kuieleza Mahakama hiyo kuwa wanatarajia kuwa na mashahidi 20 na vielelezo kadhaa.

Kusomewa kwa maelezo hayo, kunatokana na upelelezi wa kesi hiyo ya Jinai namba 196/2023 kukamilika.

Katika kesi hiyo, washtakiwa hao walikuwa wanakabiliwa na mashtaka mawili likiwemo la kwanza la unyang'anyi.

Shtaka la unyang'anyi wa kutumia silaha, washtakiwa kwa pamoja wanadaiwa kutenda kosa hilo, Oktoba 16, 2023 katika eneo la Msasani Beach.

Inadaiwa siku hiyo ya tukio, washtakiwa kwa pamoja waiiba simu ya mkononi aina ya iPhone yenye thamani ya Sh 3.5milioni; miwani moja ya macho yenye thamani ya Sh 300,000; pea moja hereni za dhahabu zenye thamani ya Sh 500,000; saa ya mkono yenye thamani ya dola za kimarekani 120.

Vingine ni mkoba na fedha taslimu Sh 100,000 vyote vikiwa mali ya Han Nooh Hussein na kwamba washtakiwa hao kabla na baada ya kufanya wizi huo, walimtishia mlalamikaji kwa bastola aina ya Glock 19, ili wajipatie vitu hivyo bila kikwazo.

Shtaka la pili ni kumteka na kumshikilia Han Hussein, ambapo wanadaiwa kutenda kosa hilo, Oktoba 16, 2023 eneo la Beach ya Msasa, lililopo wilaya Kinondoni.

Inadaiwa siku hiyo, washtakiwa walitumia nguvu na kumteka Han Hussein aende mtaa wa Ujirani uliopo Mbezi Beach na alipofika hapo, walimchukua na kumpeleka katika nyumba ya Haidary Waziri na kisha kushikilia kwa simu nne, wakati wakijua ni kinyume cha sheria.

Kwa mara ya kwanza, washtakiwa hao walifikishwa mahakamanai hapo Oktoba 30, 2023.

Hata hivyo katika kipindi chote cha kesi hiyo, washtakiwa walikuwa rumande kutokana na shtaka la unyang'anyi wa kutumia silaha kutokuwa na dhamana kwa mujibu wa sheria.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live