Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Waliokamatwa mgogoro wa ardhi waachiwa kwa dhamana

Dhamana, Hukumu Waliokamatwa mgogoro wa ardhi waachiwa kwa dhamana

Tue, 5 Dec 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

New Content Item (1) Dodoma. Watu watatu kati ya 16 waliokamatwa na Polisi kutokana na vurugu zilizozuka wakati wa maofisa upimaji ardhi walipokwenda kupima viwanja katika Mtaa wa Azimio kata ya Ipala jijini Dodoma wameachiwa kwa dhamana.

Watu watatu kati ya 16, ambao walikamatwa na Polisi Novemba 30,2023 walianza kuachiwa Desemba 2,2023 kwa dhamana huku wengine 13 wakiachiwa leo mchana.

Akizungumza leo Jumatatu Desemba 4, 2023, Mwenyekiti wa CCM wa Tawi la Azimio kata ya Ipala, Omary Juma amesema kuwa Mwenyekiti wa Mtaa wa Azimio, Seleman Ngongwai, mama mwenye mtoto wa wiki moja na mama aliyempelekea mtoto kituoni waliachiwa Desemba Mosi mwaka huu.

“Hawa wengine ndio wamerudi kutoka polisi sasa sijajua kuwa wameelezwa warejee lini tena polisi. Lakini hali sasa ni shwari watu hawakimbii tena maporini kujificha,”amesema.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Martin Otieno amesema taratibu za kisheria zinaendelea na kwamba wanapeleka jalada la mashataka kwa mwendesha mashtaka wa Serikali, ili waweze kulipitia na kama kupelekwa mahakamani basi wafanye hivyo.

“Hali ni shwari (katika mtaa wa Azimio) uelimishaji wananchi unaendelea wanatakiwa kuelimishwa tu na uelimishaji unaendelea kwenye eneo hilo,”amesema.

Desemba 2, 2023 akizungumza na Mwananchi, Mwenyekiti wa CCM tawi la Ipala, Omary Juma alisema wataalam wa upimaji walipofika wananchi walijitokeza na kuhoji ni kwa nini wamekwenda kupima bila kuwashirikisha.

Amesema hali hiyo ilisababisha vurugu kati ya wananchi na wataalam hao, zilizosababisha baadhi ya watu kukamatwa na polisi katika nyakati tofauti.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Jabir Shekimweri alisema amepata taarifa watalaam wakiwa kazini walivamiwa na wananchi na kuwafanyia vurugu, hivyo walijihami kwa kuwajulisha polisi ambao walichukua hatua.

Kuhusu wananchi kutoshirikishwa, Shekimweri alisema alifanya kikao cha pamoja kati ya kamati ya maendeleo ya kata inayoongozwa na madiwani wa kata ya Nzuguni na Ipala na kukubaliana upimaji huo kufanyika.

Amesema eneo hilo ni la Serikali chini ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma baada ya kuvunjwa kwa CDA Mei mwaka 2017.

“Kwa wananchi wa kawaida hili wanalijua kuwa tunapanga mji pale na wao tunawagaia viwanja, sisi tumeshawahakikishia hili jambo,”alisema.

Naye Mkurugenzi wa jiji la Dodoma, John Kayombo alisema fujo hizo zilitokea kwa sababu kuna baadhi ya wananchi waliuza vipande vya ardhi katika eneo hilo la Serikali bila kufuata utaratibu.

“Kuna baadhi ya watu waliuza maeneo kwa watu sasa wanadaiwa fedha warejeshe. Hawana haki yoyote kwa sababu eneo ni la Serikali. Tunapima kuanzia Nzuguni, Mahomanyika mpaka kule Ipala. Ile ilikuwa reserve (akiba) ya Serikali tuliamua kuipima viwanja,”alisema.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live