Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Walioingiza kemikali Tanzania wahukumiwa kulipa Sh100 milioni

90727 Pic+kemikali Walioingiza kemikali Tanzania wahukumiwa kulipa Sh100 milioni

Fri, 3 Jan 2020 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam imewahukumu watu saba wakiwamo watano wa familia moja, kulipa fidia ya Sh100 milioni kwa Serikali ya Tanzania, baada ya kupatikana na hatia ya kuingiza nchini kemikali bashirifu bila kuwa na kibali.

Mbali na kulipa fidia, mahakama hiyo imewahukumu kulipa faini ya Sh 500,000 kwa kila mmoja au kwenda jela miaka miwili.

Pia, Mahakama hiyo imeamuru kemikali hizo, zikiwamo dawa za viwandani na za binadamu, zitaifishwe na zikabidhiwe kwa Wakala wa Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali.

Hata hivyo, washtakiwa hao wamefanikiwa kulipa faini na fidia na hivyo kuachiwa huru.

Washtakiwa katika kesi hiyo ya jinai namba 181/2019 ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Teckno Net Scientific, Benedict Assey; Ofisa Utawala, Wenceslaus Assey; Meneja Masoko, Wilfrida Assey; Ofisa Masoko na Manunuzi Salvatory Assey.

Wengine ni Mtunza Stoo, Emmanuel Assey, Samwel Mahalila na Matilda Temba.

Washtakiwa hao wametiwa hatiani,  baada ya kukiri mashtaka yao na kumuandikia barua Mkurugenzi wa Mashtaka Tanzania(DPP) wakiomba wasamehe na wapunguziwe adhabu.

Hata hivyo, mshtakiwa wa nane katika kesi hiyo, Everling Matinga, ambaye ni Mkemia Mwandamizi wa Serikali ya Tanzania, yeye hajakiri mashtaka hayo, hivyo kesi hiyo itaendelea dhidi yake.

Akisoma hukumu hiyo leo Ijumaa Januari 2, 2020, Hakimu Mkazi, Vicky Mwaikambo amesema washtakiwa wametiwa hatiani katika mashtaka ya kufanya biashara ya kemikali bashirifu na kuingiza nchini kemikali hizo bila kuwa na kibali na kukutwa wakizimiliki.

"Mmetiwa hatiani kama mlivyoshtakiwa, hivyo kila mshtakiwa atatakiwa kulipa faini ya Sh500,000 au kwenda jela miaka miwili, pia washtakiwa wote kwa pamoja mnatakiwa kulipa fidia Serikali ya Sh100 milioni, vilevike kemikali hizo zitaifishwe na kukabidhiwa kwa Wakala wa Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali," amesema Hakimu Mwaikambo.

Awali, Mkurugenzi Msaidizi wa Mashtaka, Maternus Marandu akisaidiana na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Ladslaus Komanya alidai wanaiomba mahakama hiyo itoe adhabu kali dhidi ya washtakiwa hao kwa mujibu wa sheria.

Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, washtakiwa hao saba, wanadaiwa kati ya Mei mosi, 2016 na Mei 30, 2017, Kijitonyama wilaya Kinondoni, wanadaiwa kufanya biashara ya kemikali bashirifu yenye uzito wa lita 526.50 na kilogram  874.50 bila ya kuwa na kibali kutoka  Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali.

Katika shtaka la kuingiza kemikali hizo nchini bila kusajiliwa na kinyume cha sheria ya Kemikali za viwandani na watumiaji wa dawa, washtakiwa wanadaiwa Juni 2, 2016, katika bandari  Kavu ya AMI, washtakiwa huku wakijua kuwa wanatakiwa kusajiliwa ili waweze kuingiza kemikali hiyo, waliingiza kemikali hizo bila kusajiliwa.

Pia, wanadaiwa kukutwa wakimiliki kemikali hizo, katika maghala ambayo yalikuwa hayajasajiliwa yaliyopo maeneo ya Bagamoyo, Moshi(Kilimanjaro) na Kijitonyama.

Chanzo: mwananchi.co.tz