Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Walioiba Bilioni 2.1 Wanaswa na Iringa na Mabulungutu ya Pesa

Pesa Iringa Fedha zilizokamatwa na jeshi la Polisi Mkoani Iringa

Fri, 11 Feb 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Allan L. Bukumbi ametoa ripoti ya matukio kadhaa ikiwemo lililohusisha wizi wa zaidi ya Shilingi Bilioni mbili mkoani humo.

Jeshi la Polisi mkoani Iringa linafanya Uchunguzi/Upelelezi dhidi ya watuhumiwa wa wizi wa fedha za kitanzania kiasi cha TSh 2,129,856,000= mali ya kampuni ya SELCOM PAYTECH LIMITED ambapo wakala wa Selcom aitwaye TYSON KASISI wa mkoani Iringa kupitia huduma ya ‘Selcom Pay’ isivyo halali alihamisha fedha kwenda nambari mbalimbali za simu na kisha kuchukuliwa taslimu kupitia wakala wa huduma za kifedha za mitandao mbalimbali ya simu pamoja na akaunti za Benki.

Wizi wa fedha hizo ulifanyika kwa njia ya mtandao katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Iringa, Dar es Salaam na Morogoro kati ya tarehe 9 Novemba 2021 hadi 27 Novemba 2021 baada ya wakala huyo TYSON KASISI kufanikiwa kuchezea mfumo wa kieletroniki wa ‘Selcom Pay’ unaomilikiwa na Kampuni ya SELCOM PAYTECH LIMITED.

Wakala huyo kwa njia ya udanganyifu alianza kujitumia fedha pamoja na kuwatumia watu wengine na kwa kushirikiana na genge lake la uhalifu walifanikiwa kuiba kiasi hicho cha TSh 2,129,856,000=.



Jeshi la Polisi mkoa wa Iringa limefanikiwa kukamata (Kuokoa) fedha taslimu kiasi cha TSh 956,974,000= kutoka kwa watuhumiwa na washiriki wa uhalifu huo ambao walipokea sehemu ya fedha hizo kwa ajili ya kuzificha katika maeneo mbalimbali ikiwemo makazi na shambani.

Aidha, kiasi cha fedha za kitanzania TSh 121,215,783= zimezuiliwa katika moja ya benki za biashara mkoani Iringa ikiwa ni mazalia ya uhalifu.

Upelelezi uliofanyika mpaka sasa umebaini kuwa genge la uhalifu na wizi wa fedha za Selcom uliongozwa na watu watatu ambao ni TYSON KASISI, PATRICK CHALAMILA na EVARISTO CHALAMILA ambao wamebainika kuwa wanufaika wakuu wa uhalifu huo.

Halikadhalika, mali ambazo ni mazalia ya uhalifu zimekamatwa na kuhifadhiwa ikiwa ni magari manne (4) yenye thamani ya TSh 303,000,000= ambayo ni;



i. SCANIA yenye jina la mtuhumiwa PATRICK CHALAMILA kwa thamani ya Sh 128, 000,000=.

ii. MITSUBISH FUSO usajili namba T 796 DXV yenye jina la mtuhumiwa TYSON KASISI kwa thamani ya Sh 75,000,000=.

iii. TOYOTA HARRIER usajili namba T 719 DXX yenye jina la mtuhumiwa TYSON KASISI kwa thamani ya Sh 72,000,000=.

iv. NISSAN JUKE usajili namba T 605 DXV yenye jina la mtuhumiwa PATRICK CHALAMILA kwa thamani ya Sh 28,000,000=.

Pia imekamatwa gari Toyota IST yenye namba za usajili T 576 DRN mali ya PATRICK CHALAMILA lililotumika kufanikisha uhalifu kwa kusafirisha fedha za wizi kutoka Madibira Wilayani Mbarali na Ilula Wilayani Kilolo kwenda kuzificha Kilombero mkoani Morogoro.



Ushahidi uliokusanywa mpaka sasa umetosha kuwafikisha watuhumiwa kumi (10) Mahakamani kujibu tuhuma zinazowakabili kwa makosa ya Kuongoza Genge la Uhalifu na Kujipatia Fedha kwa njia ya Udanganyifu.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live