Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Waliochapisha maudhui mtandaoni bila kibali walipa faini, wakwepa kifungo

98170 Pic+maudhui Waliochapisha maudhui mtandaoni bila kibali walipa faini, wakwepa kifungo

Fri, 6 Mar 2020 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imewahukumu mfanyabiashara Emmanuel Sisala (32) na wenzake Juhudi Motela(29) kulipa faini ya Sh5 milioni kila mmoja au kwenda jela mwaka mmoja.

Hukumu hiyo imetolewa baada ya wawili hao kukutwa na hatia  ya kumiliki na kuchapisha maudhui mtandaoni bila kuwa na leseni ya Mamlaka ya Mawasiliano nchini( TCRA).

Sisala na Motela wanadaiwa kuchapisha maudhui kupitia televisheni ya mtandaoni iitwayo Jumo Tv bila kuwa na kibali kutoka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania ( TCRA) wakati wakijua kuwa ni kinyume cha sheria ya mtandao.

Mbali na faini, mahakama hiyo imetaifisha vielelezo 11 ambavyo ni kompyuta nne, vipaza sauti vinne, kamera moja na simu tatu aina ya aina ya Iphone6 na Sumsung ambavyo vilitumika katika kuchapisha maudhui hayo, kuwa mali ya Serikali.

Hata hivyo, washtakiwa hao wamefanikiwa kulipa faini na hivyo kukwepa kifungo cha mwaka mmoja jela.

Hukumu hiyo imetolewa leo Ijumaa Machi 6, 2020 na Hakimu Mkazi mwandamizi, Augustina Mmbando baada ya mshtakiwa kukiri shtaka lao na hivyo mahakama kuwatia hatiani.

Pia Soma

Advertisement

“Washtakiwa mmetiwa hatiani kama mlivyoshtakiwa hivyo mtatakiwa kulipa faini hiyo au kutumikia kifungo.”

“Baada ya kukiri shtaka lenu mahakama hii imewatia hatiani na kuwahukumu kulipa faini ya Sh5 milioni kila mmoja na kama mtashindwa basi kila mmoja atatumikia kifungo cha miezi 12 jela na vitu vyote walivyokamatwa navyo washtakiwa vimetaifishwa na kuwa mali ya Serikali,” amesema hakimu Mmbando.

Awali, wakili wa Serikali, Adolf Lema aliieleza mahakama kuwa kesi hiyo iliitwa kwa ajili ya washtakiwa kusomewa maelezo ya awali  na ni baada ya kukiri shtaka lao.

Kabla ya kutolewa kwa hukumu hiyo, wakili  Lema aliiomba mahakama hiyo kutoa adhabu kali dhidi washtakiwa huyo ili iwe fundisho kwa watu wengine wenye tabia ya kuchapisha maudhui  mtandaoni bila kuwa na leseni kutoka TCRA.

Pia aliomba vifaa walivyokutwa navyo washtakiwa  vitaifishwe na kuwa mali ya Serikali.

Washtakiwa walifikishwa kwa mara ya kwanza Kisutu Februari 26, 2020 wakikabiliwa na shtaka hilo katika kesi ya jinai namba 33/2020.

Hata hivyo, siku hiyo waliposomewa shtaka lao walikiri na upande wa mashtaka uliomba tarehe nyingine kwa ajili ya kuwasomewa hoja za awali.

Katika kesi ya msingi, Sisala na Motela wanakabiliwa na shtaka moja la kuchapisha maudhi katika Mtandao bila kuwa na leseni kutoka ya TCRA.

Wanadaiwa kutenda kosa hilo  kati ya Januari 2018 na Februari 2020 maeneo mbalimbali ya Jiji la  Dar es Salaam.

Inadaiwa katika kipindi hicho washtakiwa walichapisha maudhui kupitia Televisheni ya mtandaoni bila kuwa na kibali kutoka TCRA wakati wakijua kuwa ni kinyume cha sheria ya mtandao.

Chanzo: mwananchi.co.tz