Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Walimu waliomuadhibu mwanafunzi washtakiwa kwa mauaji

15440 Walimu+pic TanzaniaWeb

Tue, 4 Sep 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Bukoba. Chanzo cha walimu wawili wa shule ya msingi Kibeta kufunguliwa kesi ya mauaji ya kukusudia ni mwanafunzi Sperius Eradius ambaye sasa ni marehemu kupiga kelele akiomba msaada huku kipande cha kuni kikitumika kama mbadala wa fimbo.

Watuhumiwa hao Respicius Mtazangira na Julieth Gerald walifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mfawidhi Bukoba jana na kusomewa shtaka la mauaji huku kesi yao ikiahirishwa hadi Septemba 17.

Akizungumza na Mwananchi kuhusu sababu za watuhumiwa kufunguliwa shtaka la mauaji ya kukusudia, wakili mwandamizi wa Serikali, Athumani Matuma alisema kuwa kipande cha kuni ndicho kilitumika kumwadhibu mwanafunzi huyo wakati akipiga kelele za kuomba msaada kwa wenzake.

Katika kesi hiyo namba 18/2018, Wakili Matuma aliiambia mahakama hiyo kuwa upelelezi umekamilika huku hakimu mkazi mfawidhi, John Kapokolo akisema mahakama hiyo haina uwezo wa kusikiliza kesi za mauaji na watuhumiwa walirudishwa rumande.

Wakili huyo alisema ofisi yake inafanya utaratibu wa kuihamishia kesi hiyo Mahakama Kuu kwa ajili ya kupangiwa tarehe za kuanza kusikilizwa kwa kuwa upelelezi tayari umekamilika.

Kifo cha mwanafunzi Sperius Eradius kiligusa hisia za watu wengi kutokana na mazingira yake ambayo mwanafunzi huyo alidaiwa kuiba mkoba wa mtuhumiwa wa pili, Julieth na kudaiwa kumpeleka mwanafunzi huyo kwa Respicius anayesimamia nidhamu.

Kifo hicho pia kiliibua mgogoro kati ya Serikali na familia ya marehemu ambayo iliomba ufanyike uchunguzi huru baada ya kutoridhika na ripoti ya awali ya daktari iliyoonyesha kuwa mwanafunzi huyo alikuwa na makovu ya siku nyingi.

Serikali ilikubaliana na ombi la familia baada ya uchunguzi wa pili na marehemu alizikwa siku ya tano wilayani Muleba na mazishi yake kuhudhuriwa na naibu waziri wa Tamisemi, Josephat Kandege ambaye alitoa ubani wa Sh2 milioni.

Pia, kutokana na tukio hilo Serikali imechukua hatua kadhaa ikiwa ni pamoja na kuusimamisha uongozi wa shule na kuunda kamati ya kuchunguza kama walikuwa wanasimamia majukumu yao ipasavyo.

Chanzo: mwananchi.co.tz