Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Walimu matatani madai ya matumizi mabaya madaraka

Arrested Crime.jfif Walimu matatani madai ya matumizi mabaya madaraka

Tue, 7 Jul 2020 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

WALIMU watatu wa Shule ya Sekondari Kalenge, wilayani Biharamulo wanashikiliwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoani Kagera kwa madai ya matumizi mabaya ya madaraka.

Walimu hao wanadaiwa kuuza jina la mwanafunzi wa kidato cha nne aliyekuwa mgonjwa kwa kumfukuza kwanza shule kwa madai ya utoro na baadaye jina lake kupewa mwanafunzi mwingine ambaye alifanya mtihani na kufaulu kwa daraja la pili.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na Mkuu wa TAKUKURU Mkoa, John Joseph, walimu hao walifanya udanganyifu wakati wa mtihani wa kidato cha nne uliofanyika mwaka 2019, huku wakijua mwanafunzi aliyefukuzwa alikuwa mgonjwa.

Aliwataja walimu hao kuwa ni Mkuu wa Shule hiyo, Boniphace Eliab, Makamu Mkuu wa Shule, Edwin Valentine na Mwalimu wa Taaluma, Grevas Richard.

“Uchunguzi wa TAKUKURU ulibaini kwamba walimu hao walimfukuza shule mwanafunzi mmoja (jina limehifadhiwa) kwa kisingizio cha kuwa alikuwa mgonjwa na kisha wakati wa mitihani kwa njia za rushwa waliitumia namba yake kumpa mwanafunzi mwingine ambaye aliufanya mtihani huo,” alisema na kuongeza:

“Uchunguzi wetu umebaini pia baada ya matokeo kutoka, jina la mwanafunzi aliyekuwa amefukuzwa lilioneka kuwa amefaulu kwa kupata daraja la pili, huku inafahamika kuwa mwanafunzi halisi mwenye jina hilo alishafukuzwa na hakufanya mtihani.”

Kwa mujibu wa Joseph, hali hiyo ilimfanya mzazi wa mwanafunzi aliyefukuzwa kushikwa na mshangao na kuamua kutoa taarifa TAKUKURU.

Alisema uchunguzi ulibaini kuwa wakati mwanafunzi huyo mgonjwa wa macho ametaarifiwa juu ya kufukuzwa, uongozi wa shule kwa njia za rushwa ulimwingiza mwanafunzi mwingine (jina limehifadhiwa), ambaye alifanya mtihani wa kuhitimu kwa jina na namba ya mwanafunzi aliyedaiwa kufukuzwa.

“Matokeo yalipotoka yalionyesha jina na namba ya mwanafunzi aliyedaiwa kufukuzwa kwamba amefaulu kwa daraja la pili, huku mwanafunzi halisi akiwa hakufanya mtihani wowote,” alisema.

“Kutokana na taarifa hizo TAKUKURU iliamua kuwashikilia walimu wote kwa mahojiano zaidi,” alisema.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live