Dar es Salaam. Walimu wanne akiwemo meneja wa Shule ya Msingi na Sekondari Kings, Stella Shuma wamefikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashtaka mawili likiwemo la kufanya kazi nchini bila ya kuwa na kibali cha Idara ya Uhamiaji.
Mbali na Stella wengine ni raia wa Kenya, Ezron Maina, Ruth Frank, Joseph Kuria na Charles Sakawa.
Wakili wa Serikali, Faraji Nguka akisoma hati ya mashtaka mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Augustine Rwezile, alidai kuwa washitakiwa walitenda makosa hayo kati ya Septemba, 2018 na Machi, 2019 eneo la Goba, Wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam.
Ilidaiwa kwamba katika shtaka la kwanza, Maina, Ruth, Kuria na Sakawa katika kipindi hicho, jijini Dar es Salaam, walikutwa wakifanya kazi katika shule hiyo wakati wakijua hawana kibali kutoka Idara ya Uhamiaji.
Shitaka la pili linalomkabili Stella anayedaiwa kwamba katika kipindi na eneo lilipofanyika kosa la kwanza akiwa meneja wa Shule ya Kings aliwaajiri washitakiwa hao huku akijua ni raia wa Kenya na hawana kibali kutoka Idara ya Uhamiaji.
Washitakiwa wote walikana makosa hayo na waliachiwa kwa dhamana baada ya kutimiza sharti la kuwa na mdhamini mmoja aliyesaini bondi ya Sh5 milioni pamoja na washitakiwa hao kujidhamini wenyewe kwa kiasi hicho cha fedha.
Pia Soma
- Serikali kuikatia rufaa hukumu ya wakurugenzi kusimamia uchaguzi
- Serikali yachukua hatua ndege zake kuchelewa kuanza safari
- Serikali ya Tanzania yatoa neno ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo
- Tembo wafungwa mikanda ya GPS