Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wakurugenzi watatu kortini kwa tuhuma za kughushi zabuni ya ujenzi

95509 Pic+wakurugenzi Wakurugenzi watatu kortini kwa tuhuma za kughushi zabuni ya ujenzi

Fri, 14 Feb 2020 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar Es Salaam. Wakurugenzi watatu wa Kampuni ya CIVMARK LTD na Wakili mmoja wa kujitegemea, wamefikishwa katika Mahakama  ya Hakimu Mkazi Kisutu, kujibu mashtaka manne, likiwamo la kughushi zabuni ya ujenzi wa barabara ya Rubya- Kanyamabogo, yenye urefu wa kilomita tano, iliyopo Manispaa ya Bukoba, mkoani Kagera.

Washtakiwa hao ni Crispin Mwombeki, Joseph Nyamwero, Hadija Nyumbe, ambao ni Wakurugenzi wa Kampuni ya CivMark Ltd na Wakili wa kujitegemea, Glory Benne.

Washtakiwa hao wamefikishwa  mahakamani hapo leo, Februari 12, 2020 na kusomewa mashtaka yao, mbele ya Hakimu Mkazi, Rashid Chaungu.

Akiwasomea mashtaka yao, Wakili wa Serikali Adolf Lema, alidai kuwa washtakiwa wanakabiliwa na kesi ya jinai namba  21/2020.

Lema alidai, katika shtaka la kwanza ambalo ni la kughushi linalomkabili Mwombeki na Nyamwero, washtakiwa hao wanadaiwa kutenda kosa hilo Septemba 17, 2017 jijini Dar es Salaam.

Washtakiwa wanadaiwa siku hiyo ya tukio kwa nia ya kudanganya, walighushi mkataba wa makubaliano ya pamoja, wakionyesha kuwa Kampuni mbili ambazo ni Civmark Ltd na Mecco Ltd, zimekubaliana kuunda kampuni moja  kwa jina la CVMARK MECCO JV, kwa lengo la kupata zabuni ya kujenga barabara ya Rubya- Kanyamabogo, kitu ambacho sio kweli.

Pia Soma

Advertisement
Pia, Mwombeki,  Nyamwero na Nyumbe, ambapo wanadaiwa Septemba 20, 2017 jijini Dar es Salaam, kwa nia ya kudanganya, walighushi nguvu maalumu ya uwakilishi wa kisheria, wakionyesha kuwa Kampuni hizo mbili, wamekubaliana kutoa uwakilishi kwa Joseph Nyamwero kuwawakilisha katika  zabuni hiyo, kitu ambacho sio kweli.

Shtaka la tatu, Mwombeki anadaiwa Oktoba 10, 2017, katika Manispaa ya Bukoba mkoani Kagera, kwa nia ya kudanganya, alighushi nyaraka akidanganya kuwa Kampuni ya MECCO LTD imekubali kutoa nguvu maalum ya uwakilishi wa kisheria kwa Nyamwero kuiwakilisha kampuni hiyo katika zabuni ya ujenzi wa barabara ya Rubya- Kanyamabogo, kwa kiwango cha lami, yenye urefu wa kilomita tano, iliyopo Manispaa ya Bukoba mkoani Kagera.

Pia mshtakiwa huyo, anadaiwa siku na eneo hilo, alighushi nyaraka akionyesha Kampuni ya MECCO LTD, imejiweka wazi ina uwezo wa kutekeleza zabuni ya ujenzi wa barabara ya Rubya- Kanyamabogo.

Washtakiwa baada ya kusomewa mashtaka yao walikana na Wakili anayewatetea, Pascal Kamala, aliomba mahakama iwapatie dhamana wateja wake.

Hakimu Chaungu, alitaja masharti ya dhamana ambayo ni kila mshtakiwa kuwa na mdhamini mmoja mwenye barua kutoka Serikali ya Mitaa, anayetambulika kisheria.

Pia kila mdhamini anatakiwa kusaini bondi ya Sh5 milioni.

Washtakiwa wapo nje kwa dhamana, baada ya kukamilisha masharti hayo ya dhamana.

Hakimu Chaungu, ameahirisha kesi hiyo hadi Februari 26, itakapotajwa.

Chanzo: mwananchi.co.tz