Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wakulima, wafugaji, Kilindi wamaliza tofauti, watangaza amani

Kilindi Pic Data Wananchi wakiwa katika kikao cha amani

Tue, 15 Mar 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wananchi wa viijiji vya Elerai na Kibirashi ambavyo kulitokea mapigano ya wakulima na wafugaji Januari mwaka huu wametangaza kuanza ushirikiano upya katika shughuli zao baada ya kupatanishwa na viongozi wa wilaya na mkoa.

Kauli hiyo imetolewa leo Jumanne Machi 15, 2022 na sheikh wa Mkoa wa Tanga, Ally Luwuchu kwenye kikao cha amani kilichoitishwa na kamati ya ulinzi na usalama ya Wilaya ya Kilindi kilichoshirikisha viongozi wa dini.

Sheikh Luwuchu amesema alitembelea vijiji vyote viwili yeye na viongozi wenzake wa madhehebu mengine ya dini kuhamasisha kurejesha amani kwenye maeneo hayo, ambapo walimuahidi kumpa mrejesho na baadae kutuma mjumbe kuwa wamekubali.

Katika kikao cha kuwakutanisha wananchi hao Sheikh alitoa ujumbe wa amani kwa uliotoka Elerai na baadae wananchi wa Kibirashi nao kukubali kupatanishwa huko.

"Nashukuru sana mmenitamkia kwamba upande wenu (Elerai) mmetuma salamu kwamba wamasai mmesamehe na hakuna tatizo, sasa niulize upande wa Kibirashi na nyie mnasemaje hakuna tatizo, nashukuru kama sote tumekubaliana katika hili", amesema Sheikh Luwuchu katika mkutano huo.

SOMA:Watano wafariki dunia mapigano ya wakulima, wafugaji Tanga

Advertisement Mchungaji Hellena Ndingaba wa kanisa la Pentecost Kibirashi kwa upande wake amewataka wazazi kuhakikisha wanapandikiza mbegu ya upendo kwenye familia zao, hali hiyo itaweza kusaidia kuepuka kutokea migogoro kwani familia itakuwa inamjua Mungu.

"Nasisitiza endapo wazazi wa kila familia atafundisha na kusimamia watu wake wamjue mungu, changamoto ya kulipa visasi haitakuwepo kwa kila mmoja kumjua Mungu na upendo ndani yao, niwasihi wazazi msimamie sana familia zenu zimjue Mungu", amesema Mchungaji Hellen.

SOMA:20 washikiliwa mapigano ya wakulima, wafugaji Kilindi

Awali kwenye mkutano huo mkazi wa Kibirashi, Pili Juma amesema kuna madhara wameyaona wao kama wanawake ikiwemo waume zao na vijana kuzitoroka familia, hivyo upo umuhimu wa kupatanishwa ili ushirikiano uwepo kama awali na wanaume kurudi kwenye familia zao.

"Wanaume nyie mnaanzisha vita halafu mambo yakiharibika mnazikimbia familia zenu na kwenda kujificha, wanaopata shida kwenye vita ni sisi wanawake na watoto wetu kwasababu tunashindwa kukimbia na familia,naunga mkono makubaliano haya ya amani na ushirikiano baina yetu", amesema Pili.

Mkazi wa Elerai, William Toroka amema kuwa katika kijiji chao huduma nyingi muhimu wanategemea Kibirashi hivyo kitendo cha kutoelewana ilileta madhara kupata huduma.

Ofisa mwandamizi Shirika la World Vision Tanzania, Ajabu Mtweve ameishukuru Serikali kwa kuwaruhusu kusimamia utekelezaji wa vikao ya kuleta amani Kilindi, kwani wao husimamia haki za mtoto na katika tukio hilo mtoto mmoja aliuwawa hivyo wao kama wadau waliguswa na tukio hilo.

Akifunga kikao hicho katibu tawala Wilaya ya Kilindi, Walda Maulid kwa niaba ya mkuu wa wilaya hiyo Abel Busalama, amesema walishaunda timu ya kusimamia mchakato wa amani kwenye maeneo husika na kazi bado inaendelea kuhakikisha amani inarejea kwenye maeneo hayo.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live