Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wakulima tisa wakatwa mapanga Siha, saba wakamatwa

Wakulima Tisa Wakatwa Mapanga Siha, Saba Wakamatwa Wakulima tisa wakatwa mapanga Siha, saba wakamatwa

Tue, 12 Jul 2022 Chanzo: www.mwananchi.co.tz

Wakulima tisa wametajwa kujeruhiwa kwa kukatwa mapanga baada ya kuibuka mapigano yaliyotokana na makundi ya vijana wa kimasai (Morani) kutoka Wilaya ya Longido mkoani Arusha kuingiza mifugo kwenye mashamba ya wakulima.

Morani hao wamevamia maeneo ya wakulima ya West Kilimanjaro Wilaya Siha na kuharibu zaidi ya ekari 1,800 za ngano na Maharage kwa kulishia mifugo yao huku wakijeruhi kwa mapanga wakulima wanaowazuia.

Kutokana na hali ilivyo katika eneo hilo, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Stephen Kagaigai ameliagiza Jeshi la Polisi kuhakikisha linawadhibiti wafugaji hao akisema kamati ya usalama mkoa itakutana haraka hali suala.

Kagaigai alieleza kuwa kikao hicho kitajadili kwa kina hali ilivyo na kuweka mikakati ya kuwadhibiti wafugaji hao huku akitishia kutumia Jeshi kudhibiti morani na ng’ombe ambao wamefanya uharibifu mkubwa.

Mkuu huyo wa mkoa amemwagiza Kamanda wa Polisi mkoani humo, Simon Maigwa kushirikiana na mshauri wa mgambo wa mkoa (JWT) kuona namna ya kudhibiti wafugaji hao akisema Serikali haitavumilia kuona uharibifu huo ukiendelea.

Akizungumza baada ya kutembelea mashamba hayo na kuona uharibifu uliofanyika, mkuu huyo wa mkoa alionyesha kusikitishwa na kitendo hicho na kusema hatavumilia kuona uharibifu huo ukiendelea akitaka ukome mara moja.

“Niwape pole kwa kilichotokea na inasikitisha. Nilipokea taarifa kutoka kwa mkuu wa wilaya, nikuwepo. Haiwezekani tukae na watu wasiothamini mali za watu wengine, Serikali haiwezi kukubaliana na kitu kama hicho.

“Lazima sheria ichukue mkondo wake. RPC hakikisha waliokutwa na mifugo kwenye mashamba haya ya wakulima sheria ichukue mkondo wake,” alisema Kagaigai ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Usalama Mkoa wa Kilimanjaro.

Alisema kamati ya usalama ya mkoa na kamati ya usalama wilaya zitakaa kuona mikakati gani iwekwe ikiwezekana itumike nguvu ya Jeshi kuzuia hali hiyo.

Alimwagiza Mkuu wa Wilaya ya Siha kuwasiliana na Mkuu wa Wilaya ya Longido kuangalia namna ya kushughulika na wafugaji hao huku akisema kama wamekuja kufanya vurugu, hawatakaa kimya ni lazima wawashughulikie.

Kagaigai alimtaka RPC kuhakikisha muda wote magari yanakuwa na mafuta kwa ajili ya doria na kuwadhibiti wafugaji hao .

“Tuko tayari kuleta jeshi la wananchi kulinda haya maeneo hatuwezi kuendelea kupata hasara kiasi hiki,” alisema.

Kwa upande wake, Kamanda Maigwa alisema tayari wanawashikilia wafugaji saba na kwamba waliofanya uhalifu huo lazima wakamatwe wote.

Alisema katika tukio hilowakulima walijeruhiwa.

Wakulima wafunguka

Wakizungumza kwa nyakati tofauti na ujumbe uliongozwa na mkuu wa mkoa, wakulima hao walidai huvamiwa usiku na kupigwa na wafugaji.

Akizungumza na Mwananchi, Fausta Ally, mkulima wa ngano eneo la West Kilimanjaro alisema wafugaji hao wamekuwa kero kiasi cha kuwafanya hata wawekezaji wakubwa kukimbia eneo hilo.

“Inaumiza, mpaka sasa sijui hatima yangu, mkopo niliouchukua benki nitaurudishaje, maana mazao yangu yameliwa na nililima ekari 200. Ekari 100 zote zimeliwa na hizi zilizobaki sijui hatma yake,” alisema huku akiangua kilio.

Alisema; “Serikali iangalie namna ya kutusaidia, waziri wa kilimo kipindi kile alituhamasisha tulime ngano, tumelia, kinachoumiza zaidi tumekopa na tumeingia mkataba na TBL,” alisema Ally.

Diwani wa Ngarenairobi, Patrick Kimario alisema,“Kuna vurugu kubwa. Wafugaji wanalazimisha kuingiza mifugo kwenye mashamba ya wakulima mchana na usiku na wanawapiga. Imefika mahali tunavuna mazao mabichi, ili yasiliwe na ng’ombe.”

Alisema hali ni mbaya; “Naweza kusema hii ni vita baridi, hatulali nyumbani, tunakesha mashambani kuchunga kilichopo, asilimia 90 tuna mikopo kwa ajili ya kilimo lakini hatuna tunachovuna.”

Mkulima mwingine, John Moshi alisema; “hapa nilipo sijui hatma yangu nilikopa benki kwa kuweka rehani nyumba, nikishindwa si ndiyo imeondoka!” alisema.

Mifugo yakamatwa

Jana mifugo 1,450 imekamatwa na kati ya hiyo, mbuzi na kondoo wako 965 na ng’ombe 485 huku mkuu huyo wa mkoa akiagiza isiachiliwe mpaka sheria itakapochukua mkondo wake.

“Tunataka kujua hatima ya hawa wakulima ambao mazao yao yameliwa, wenye mifugo hatuwaoni,” alisema RC Kagaigai.

Chanzo: www.mwananchi.co.tz