Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wakili wa Serikali akwamisha kesi mahakamani

Mon, 15 Apr 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Kesi inayomkabili mfanyabiashara Mustapha Kambangwa imeshindwa kuendelea baada ya wakili wa Serikali Mwandamizi, Patric Mwita kutofika mahakamani kwa kile kilichodaiwa amepata udhuru.

 Kambangwa anakabiliwa na mashtaka manne, ambayo ni pamoja na la kuisababishia Mamlaka ya Mapato Tanzania(TRA) hasara ya Sh188.9 bilioni kwa kupitia mashine ya kielektroniki (Efds).

Wakili wa Serikali, Easter Martine ameieleza mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu leo Jumatatu Aprili 15,2019 kuwa shauri hilo lilikuja kwa ajili ya kujibu hoja na wakili anayeendesha kesi hiyo ni wakili Mwita ambaye amepata udhuru.

“Kinachojitokeza mheshimiwa siku ya shauri hilo linapokuja mahakamani upande wa utetezi au mashtaka unakosekana hivyo shauri linashindwa kuendelea,” amedai Martine.

Baada ya maelezo hayo, Hakimu Mkazi, Janeth Mtega ameahirisha shauri hilo hadi Aprili 25, 2019 itakaporudi kwa ajili ya kujibu hoja.

Hoja hizo ziliwasilishwa na Wakili wa Utetezi , Samweli Shedrack aliyedai kuwa shtaka la utakatishaji wa fedha limekosewa hivyo aliiomba mahakama hiyo kuliondoa.

Katika kesi ya msingi, mshtakiwa anakabiliwa na mashtaka manne aliyoyatenda katika siku tofauti kati ya Juni Mosi ,2016 na Novemba 2, 2018 katika shtaka la kwanza, Kambangwa alijifanya kama mtu aliyesajiliwa kuwa mlipa kodi ya ongezeko la thamani (VAT).

Katika tarehe tofauti kati ya Juni Mosi,2016 na Novemba 2, mwaka huu maeneo ya Dar es Salaam kwa vitendo vya makusudi vya kukwepa kodi alitumia mashine ya kieletroniki ya EFD na huku akijua kwamba hajasajiliwa kama mlipakodi ya VAT aliisababishia TRA hasara ya 188,928,752,166.

 



Chanzo: mwananchi.co.tz