Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wakili kizimbani kwa madai ya kujipatia fedha kwa udanganyifu

94753 Wakili+pic Wakili kizimbani kwa madai ya kujipatia fedha kwa udanganyifu

Thu, 6 Feb 2020 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Wakili wa kujitegemea, Abdul Lyama mkazi wa Mbezi Makonda amefikisha katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu akikabiliwa na mashtaka matatu likiwemo la kujipatia Dola 26,250 za Kimarekani sawa na zaidi ya Sh60 milioni kwa udanganyifu.

Akisoma hati ya mashtaka wakili wa Serikali, Grory Mwenda amedai mshtakiwa huyo anakabiliwa na shtaka la kuunda genge la uhalifu, utakatishaji wa fedha na kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.

Akizungumza mahakamani hapo leo Alhamisi Februari 6, 2020, Mwenda amedai kati ya Januari Mosi, 2019 na Desemba 30, 2019 jijini Dar es Salaam mshtakiwa akiwa pamoja na wenzake ambao hawakuwepo mahakamani waliunda genge la uhalifu huku akijua kufanya hivyo  ni kosa la kisheria.

Katika shtaka la pili tarehe hiyo jijini Dar es Salaam mshtakiwa akiwa pamoja na wenzake ambao hawapo mahakamani hapo walijipatia dola za kimarekani 26, 250 ambazo ni zaidi ya Sh60 milioni wakijua fedha hizo ni zao la jinai la kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu

Katika shtaka la mwisho imedaiwa walijipatia kiasi hicho cha fedha kutoka kwa Yasser Moawed Abdelhamad wakimdanganya kumuuzia tani 25 za madini aina ya shaba huku wakijua sio kweli.

Mwenda amedai upelelezi bado haujakamilika na  kuomba mahakama hiyo kupanga shauri hilo kuendelea  Februari 10, 2020 ili waweze kuwaunganisha washtakiwa wengine ambao wapo mahabusu.

Pia Soma

Advertisement
Baada ya maelezo hayo Hakimu mwandamizi, Augustina Mmbando ameahirisha shauri hilo hadi Februari 10, 2020 itakapokuja kwa ajili ya kutajwa.

 

Chanzo: mwananchi.co.tz