Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wakili ataka kesi ya Mo Dewji kuendelea, aeleza sababu mbili

87898 Moopic Wakili ataka kesi ya Mo Dewji kuendelea, aeleza sababu mbili

Fri, 13 Dec 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Upande wa utetezi katika kesi ya kutekwa kwa mfanyabiashara maarufu nchini Tanzania, Mohamed Dewji maarufu Mo umeiomba mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuendelea na kesi hiyo kwa kuwa mshtakiwa ambaye ni dereva taxi, Mousa Twaleb amekaa mahabusu muda mrefu.

Mbali na Twaleb kukaa mahabusu muda mrefu, pia umeeleza kuwa  washtakiwa wengine katika kesi ambao ni raia wa Msumbiji na Afrika Kusini bado hawajakamatwa.

Hayo yameelezwa leo Jumanne Desemba 10, 2019 mahakamani hapo na wakili wa utetezi, Mafulu Mbagwa mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi baada ya wakili wa Serikali, Glory Mwenda kueleza upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika.

Wakili Mbagwa amedai  mshtakiwa huyo amekaa mahabusu  muda mrefu na washtakiwa wengine wako nje ya nchi, kwamba kama uwezekano wa kuwakamata haupo kesi hiyo iendelee.

"Tumekuwa tukisisitiza mshtakiwa amekaa ndani muda mrefu na kuna washtakiwa wako nje ya nchi na walieleza wametoa hati ya kuwakamata tumeomba nakala lakini hatujapewa,” amesema wakili Mbagwa.

Awali, mahakama hiyo ilitoa hati ya kuwakamata washtakiwa hao ambao ni Henrique Simbine, Daniel Manchice, Issac Tomo na Zacarious Junior (wote raia wa Msumbiji) na Phila Tshabalala ambaye ni raia wa Afrika Kusini.

Hadi sasa aliyefikishwa mahakamani ni Twaleb pekee.

Hakimu Shahidi ameahirisha kesi hiyo  hadi Desemba 23,mwaka huu.

Katika kesi hiyo inadaiwa Mei Mosi na Oktoba 10, 2018 katika maeneo ya jiji la Dar es Salaam na Johannesburg Afrika Kusini, kwa makusudi washitakiwa wote kwa pamoja waliendesha genge la uhalifu.

Inadaiwa Oktoba 11, 2018 maeneo Hoteli ya Colloseum wilayani Kinondoni Dar es Salaam, Twaleb pamoja na watu wengine ambao hawapo mahakamani, walimteka nyara Mo kwa nia ya kumhifadhi kwa siri na kumuweka maeneo ambayo ni hatari.

Kilichojiri kesi ya kumteka Mo Dewji mahakamani

Pia inadaiwa Julai 10, 2018 maeneo ya Mbezi Beach wilayani Kinondoni, Dar es Salaam, Twaleb alitakatisha fedha ambazo ni Sh8 milioni wakati akijua fedha hizo ni kosa la kushiriki genge la uhalifu na makosa ya kupanga.

Mo Dewji azungumzia siku tisa za kutekwa kwake

Mo alitekwa nyara Oktoba 11, 2018 alfajiri maeneo ya Hoteli ya Colloseum wakati akienda kufanya mazoezi na alipatikana Oktoba 20, 2018 katika eneo la Gymkhana.

Chanzo: mwananchi.co.tz