Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wakili ahoji ndugu wa watuhumiwa kuzuiwa kuingia mahakamani

58944 Wakilipic

Wed, 22 May 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mwanza.  Deo Mgengeli, wakili wa upande wa utetezi katika kesi ya jinai namba 1/2019 ya kusafirisha shehena ya dhahabu kilo 319 yenye thamani ya Sh27.18bilioni  inayowakabili watu wanane,  amelalamikia kitendo cha ndugu wa washtakiwa kuzuiwa kuingia mahakamani kusikiliza shauri hilo.

Akizungumza leo Jumanne Mei 21, 2019 katika mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Mwanza, Mgengeli amesema mahakama hiyo imeporwa uhuru wake wakati akieleza haki ya ndugu wa washtakiwa hao waliokuwa askari polisi jijini Mwanza.

"Hii mahakama ni ya wazi na mhimili wa mahakama upo huru kama ilivyo mihimili mingine na ina taratibu zake utendaji. Inaruhusu watu kusikiliza na kuhudhuria lakini kwa sasa mahakama yako imetekwa na polisi.”

"Ndugu wa wateja wetu hawaruhusiwi kuingia wala kusogelea mahakama hii,  mazingira yamekuwa sehemu ya polisi na watu wa usalama. Tunafanya kazi kwenye hofu ya mitutu,” amesema Mgengeli.

Ameongeza, “Ikizingatiwa kesi inayowakabili ni ya jinai, tunaomba mahakama yako irudishe haki hii inayopokonywa, waruhusiwe ndugu, jamaa na marafiki wa hawa washtakiwa waingie waone kinachoendelea.”

Baada ya kutoa malalamiko hayo mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi,  Rhoda Ngimilanga,  upande wa mashtaka ukiongozwa na mkurugenzi wa makosa ya rushwa na utakatishaji fedha katika ofisi ya mkurugenzi wa mashtaka (DPP),  Fredrick Manyanda amesema licha ya kifungu cha 186 (1) cha sheria ya mwenendo wa sheria ya jinai kutoa  mwongozo wa jumla kuruhusu uhuru wa mahakama lakini kuna mbadala wake.

Pia Soma

Amesema kulingana na uwape wa askari hao mahakamani ni kwa sababu za kiusalama na kuiomba mahakama kupuuza madai  hayo na kuendelea na usikilizaji wa kesi.

Baada ya mvutano wa kisheria Hakimu Ngimilanga amesema atatoa uamuzi baada ya kumaliza  kusikiliza shauri hilo.

Kesi hiyo inawakabili aliyekuwa mkuu wa operesheni mkoa wa Mwanza, Morice Okinda, E. 6948 D/CPL. Kasala, F. 1331 PL. Matete, G. 6885 D/C Alex na G. 5080 D/C Maingu.

Wengine ni G. 7244 D/C Timothy, G. 1876 D/C Japhet, H. 4060 D/C David Kadama ambao walifikishwa mahakamni hapo kwa mara ya kwanza Januari 11 mwaka huu.

Wote kwa pamoja wanakabiliwa na makosa matano ya kutakatisha fedha, uhujumu uchumi na kula njama za kupanga uhalifu, makosa wanayodaiwa kuyatenda kati ya Januari 4 na 5 mwaka huu.

Waliokwepa kifungo ni wafanyabiashara Hassan Sadiq ambaye alikuwa mshtakiwa wa kwanza katika kesi hiyo, Emmanuel Mtemi, Kisabo Nkinda na Sajid Hassan.

Chanzo: mwananchi.co.tz