Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wakili aeleza mshitakiwa alivyouza nyumba ya bil 1/

89d55e8c0524a1b59d9bf5c1a7c95de4 Wakili aeleza mshitakiwa alivyouza nyumba ya bil 1/

Wed, 16 Sep 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

WAKILI wa Kujitegemea, Majura Magafu ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam namna mwanasiasa Salma Mtambo alivyouza nyumba ya marehemu baba yake iliyopo eneo la Kariakoo jijini Dar es Salaam, iliyokuwa na thamani ya Sh bilioni moja.

Akiongozwa na Wakili wa Serikali, Faraji Ngukah, Magafu alidai mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi kuwa kati ya mwaka 2008, 2012 na 2013, mshitakiwa Mtambo alimweleza kuwa ameteuliwa na Mahakama ya Mwanzo ya Kariakoo kuwa msimamizi wa mirathi ya marehemu baba yake, Nassoro Simba.

Alidai kuwa Mahakama hiyo ilimteua kusimamia mirathi ya nyumba namba 14 iliyopo kwenye kiwanja namba 47, baada ya kuona aliyekuwa msimamizi wa awali, aliyemtaja kwa jina moja la Mboni, kuwa afya yake imedhoofika.

Magafu alidai kuwa mshitakiwa huyo, alimweleza kuwa alijitokeza Asha Mwinyimvua, akidai apewe robo ya mali alizoacha marehemu mume wake, Simba, kwa sababu aliolewa lakini hakubahatika kuzaa naye.

Wakili huyo alidai katika maelezo ya Mtambo, alimueleza kuwa baada ya mazishi ya baba yake (Simba), Mwinyimvua alidai kuwa hatodai mali zilizoachwa na marehemu mume wake.

“Alinieleza kuwa baada ya mazishi Mwinyimvua, alidai kuwa katika mali alizoacha mume wake apewe robo ya mali, ndipo wakalazimika kufungua kesi Mahakama Kuu kwa kuwa yeye hakubahatika kuzaa naye alistahili kupewa moja ya nane ya mali hizo,” alidai Magafu.

Alidai kuwa baada ya kuona Mwinyimvua anadai robo ya mali hizo, alishirikiana na mshitakiwa Mtambo, kuwatafuta mashehe ili waangalie sheria na taratibu za dini ya Kiislamu zinasemaje.

“Kwa bahati mbaya wakati tunaendelea kufuatilia suala hilo, Mwinyimvua alifariki na baadaye alijitokeza mtoto wake, Kassim Chuma aliyetaka alipwe robo ya mali alizokuwa akidai mama yake.

Baada ya kuona Chuma amejitokeza kudai mali hizo ndipo Mtambo alichoka na kulazimika kutafuta mteja wa kununua nyumba iliyopo Kariakoo ambayo ilikuwa na thamani ya shilingi bilioni moja,”alidai.

Alidai kuwa Mei 4, 2013 mshitakiwa huyo alipata mteja wa kununua nyumba hiyo, ambaye ni Nassoro Zahoro na walikubaliana alipe kwa awamu tatu na awamu ya kwanza alilipa Sh milioni 100.

Pia alidai Mei13, 2013 mshitakiwa huyo alimfuata akitaka amthibitishie mkataba wa mauziano kati yake na aliyenunua nyumba hiyo, Zahoro.

Alidai awamu ya pili, Zahoro alilipa Sh milioni 200 kisha walikubaliana katika mkataba huo endapo mnunuzi atashindwa kumalizia Sh milioni 700 Mtambo atalazimika kutafuta mteja mwingine, ili baadaye aweze kumrudishia Sh milioni 300 milioni.

Hatahivyo, Majura aliiomba mahakama hiyo ipokee kielelezo hicho (Mkataba wa Mauziano) ili kitumike kwenye ushahidi wake. Baada ya kueleza hayo, Wakili wa Serikali, Ngukah alidai kuwa upande wa mashitaka umefunga ushahidi wake.

Hakimu Shaidi aliahirisha kesi hiyo hadi Septemba 24, mwaka huu kwa ajili ya uamuzi. Mtambo ambaye alikuwa mgombea ubunge wa Korogwe Mjini mwaka 2015 kwa tiketi ya ACT Wazalendo, yupo nje kwa dhamana.

Mshitakiwa mwingine katika kesi hiyo ya jinai namba 101/2018 ni Mwanasheria wa Kujitegemea, Mohamed Majaliwa. Washitakiwa hao wanakabiliwa na mashitaka matano, yakiwemo ya kughushi sahihi za ndugu zake katika hati ya kiapo, kujipatia Sh bilioni moja kwa njia ya udanganyifu na kutotii amri halali ya Mahakama.

Chanzo: habarileo.co.tz