Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wakili Tanapa, hakimu kizimbani kwa mashtaka 11 Arusha

56064 PIC+WAKILI

Tue, 7 May 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Arusha. Wakili wa Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa), Maneno Mbunda, Hakimu wa Mahakama ya Wilaya ya Arumeru, Bernard Nganga na watu wengine watatu jana walipandishwa kizimbani kujibu mashtaka 11 ikiwemo ya kula njama na kufanya uhalifu.

Wengine waliofikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Arusha ni wakili wa Serikali, Fortunatus Muhalika, Nelson Kangero na Tumaini Mdee.

Mwendesha mashtaka mkuu wa Serikali, Javelin Rugaihuruza akisaidiwa na waendesha mashtaka waandamizi wa Serikali, Shedrack Kimaro na Theophil Mutakyawa walidai mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Niku Mwakatobe kuwa watumiwa hao walifanya makosa hayo kati ya Juni Mosi, 2018 na Aprili 15, mwaka huu.

Katika kesi hiyo ya uhujumu uchumi namba 34 ya mwaka 2019, Rugaihuruza alidai washtakiwa Kangero na Mdee kwa pamoja wakiwa siyo watumishi wa Serikali walishiriki kwa makusudi kula njama kufanya kosa kwa ajili ya kupata manufaa kinyume cha sheria.

Katika shtaka la pili linalowakabili Mbunda, Nganga na Muhalila, wanadaiwa kuomba rushwa ili kuzuia haki kutendeka huku wakijua ni kosa.

Mshtakiwa wa kwanza na wa tano wanadaiwa kutoa rushwa kiasi cha Sh31.5 milioni kwa ajili ya kumtoa Kangero ambaye alikuwa na kesi ya kukutwa na meno ya tembo yenye thamani ya zaidi ya Sh100 milioni ili kuzuia haki kutendeka.

Habari zinazohusiana na hii

Katika shtaka la nne, Mbunda, Nganga na Muhalila wanashtakiwa kwa sheria ya kuzuia rushwa chini ya sura 15(1)(a) na (2) namba 11 ya mwaka 2007 ikidaiwa waliomba na kupokea rushwa ya Sh31.5 milioni kutoka kwa Kangero na Mdee.

Mashtaka mengine ni kosa la kuharibu ushahidi kinyume na sheria ya kuharibu ushahidi sura 109 na sura 35 ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai sura ya 16 ya mwaka 2002.

Pia, wanadaiwa kuandaa hati za uongo zikiwa na lengo la kumpa mtuhumiwa dhamana kwa kuandika thamani ya nyara alizokutwa nazo kuwa na thamani ya Sh9.8 milioni wakati wakijua si kweli. Washtakiwa hawakutakiwa kujibu chochote na kesi hiyo imeahirishwa hadi Mei 20 huku wakirudishwa rumande.



Chanzo: mwananchi.co.tz