Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wakili Madeleka aibua jambo kesi ya mauaji, Mahakama yamjibu

Peter Madeleka Sds Wakili Madeleka aibua jambo kesi ya mauaji, Mahakama yamjibu

Mon, 15 Jan 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wakili Peter Madeleka, ameibua dosari alizoziita za kisheria katika hukumu dhidi ya Patrick Mmasi (25) aliyehukumiwa kifungo cha miaka 10 jela kwa kumuua mama yake bila kukusudia, baada ya nakala ya hukumu kutoonyesha adhabu hiyo.

Hukumu hiyo ilitamkwa kortini na Jaji Angaza Mwipopo wakati akitoa hukumu ya kesi hiyo namba 164/2022 Desemba 15, 2023.

Lakini nakala ya hukumu iliyochapwa na kugongwa mhuri wa mahakama, haionyeshi adhabu hiyo ya miaka 10 jela.

Hili limebainika wakati Mmasi anayetetewa na wakili Madeleka alipowasilisha kusudio la kukata rufaa kupinga kutiwa hatiani na adhabu na kupewa nakala hiyo, ili aweze kuandaa sababu za rufaa, ndipo wakili wake alipobaini dosari hiyo.

Akizungumza na gazeti hili jana, Wakili Madeleka alidai kasoro ya hukumu hiyo kutoonyesha adhabu aliyopewa mshitakiwa, kunaifanya hukumu yote kuwa batili, kwa sababu inakosa taarifa muhimu ambazo mteja wake atazitumia katika kukataa rufaa.

“Hicho alichokisema Jaji (kifungo cha miaka 10 jela) hakipo kwenye nakala ya hukumu. Hilo ni kosa kisheria kutotoa adhabu. Kutiwa hatiani ni jambo moja, lakini hakuna adhabu, ina maana pale Jaji alikuwa hasomi alichoandika,” alidai wakili Madeleka.

Alichokisema Msajili wa Mahakama

Hata hivyo, akizungumza na gazeti hili ofisini kwake Jijini Arusha jana, Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, Fredrick Lukuna alisema Jaji yuko sahihi kwa sababu hukumu na adhabu ni vitu viwili tofauti na kwamba, hukumu ikishatolewa ndipo adhabu inafuata.

Lukuna alisema baada ya Jaji kumtia hatiani Mmasi, alisikiliza maombi ya pande zote mbili ndipo akatoa adhabu na kama kungekuwa hakuna hati ya kifungo, hata Mkuu wa Gereza angelalamika kwa sababu angeshindwa kumpokea mtu asiye na hati ya kifungo.

"Jaji yuko sahihi. Alimtia hatiani baadaye akasikiliza maombi ndiyo maana mshitakiwa yuko gerezani na hati ya kifungo ilishapelekwa na hajalalamika mkuu wa Gereza kusema kwamba mmeniletea mtu ambaye hana hati ya kifungo," alisema.

"Ile hukumu haina tatizo lolote. Hukumu na adhabu ni vitu viwili tofauti. Kwa mfano, nikimtia mtu hatiani baadaye anakuja kufanya maombi, unasikia upande wa mashitaka unasema tunaomba apewe adhabu kali,” alisema na kuongeza:

“Na mshitakiwa yeye anasema mimi kutokana na hali ilivyo, naomba nipunguziwe adhabu nina watoto wananitegemea, sijui nimekuwa mwaminifu kila siku nafika mahakamani na kadhalika.’’

"Unapotoa adhabu unakuta hukumu umeshaiandika. Hukumu inatangulia halafu inafuata adhabu, ndiyo maana unaona hii hukumu amemtia hatiani, lakini baadaye akatoa adhabu, kwa hiyo sasa hivyo vyote visingekuwepo tungepata malalamiko.”

“Tungepata lalamiko kutoka kwa Patrick au bwana jela, aseme huyu mteja mliyemleta hapa mimi nashindwa kumpokea kwa sababu hakuna hati ya kifungo, lakini vyote hivyo vilifanyika kwa hiyo Jaji alikuwa sahihi,” alisisitiza Naibu Msajili huyo wa mahakama.

Tukio la mauaji lilivyokuwa

Mmasi alishitakiwa kwa kumuua mama yake mzazi, Ruth Mmasi aliyekuwa mfanyabiashara na mkazi wa Njiro kwa kumtoboa shingo kwa rato kisha kumvunja shingo na kutupa mwili wake ndani ya shimo la maji taka lililopo nyumbani kwao.

Ruth alipotea tangu Desemba 11, 2021 hadi mwili wake ulipokutwa katika shimo hilo Desemba 27,2021, ukiwa umefunikwa na shuka na mifuko ya plastiki ya kuweka mbolea.

Baada ya kusikiliza ushahidi wa mashahidi 14 wa upande wa mashitaka na Mmasi kujitetea mwenyewe, Jaji alimtia hatiani kwa kosa la kuua bila kukusudia kwa kuwa kiini cha mauaji hayo ni ugomvi na adhabu hiyo itakuwa fundisho kwa watu wengine.

Ushahidi uliomtia hatiani

Jaji alifafanua ushahidi wa mazingira kuwa umeonyesha Patrick ndiye alikuwa mtu wa mwisho kuwa na marehemu na kwa mujibu wa mashahidi sita, walieleza kwa nyakati tofauti mahakamani hapo kuwa Patrick alikiri kumuua mama yake.

Mbali ya kukiri, ushahidi unaonyesha alikwenda nao nyumbani kuonyesha mahali alipoficha rato, nyundo na simu ya mama yake aliyokuwa ameitupa kwenye shimo hilo.

"Matendo ya mshitakiwa kabla na baada ya tukio hakuonyesha anajutia yale aliyoyafanya. Alijaribu kuzuia damu isitoke shingoni kwa kumfunga shuka lakini aliposikia honi ya gari akachukua shuka zilizokuwa kwenye kamba akamfunga na kumtupa kwenye shimo la maji taka," alisema Jaji Mwipopo katika hukumu yake.

Alisema mshitakiwa huyo aliyekuwa anakabiliwa na kesi ya mauaji na baada ya kusikiliza ushahidi wa pande zote mbili, Mahakama iliona ameua bila kukusudia na mwili wa marehemu ulionyesha umechomwa shingoni na kitu chenye ncha kali.

"Marehemu alikuwa na majeraha mawili shingoni, tukio lile ni baya na ni mbaya zaidi kulifanya kwa mama yako mzazi, mwanaume hahitaji kumpiga mwanamke kwa namna yoyote, nampa adhabu ya kifungo cha miaka 10 jela," alieleza Jaji Mwipopo.

Akisoma mwenendo wa kesi hiyo ikiwemo mashahidi wa Jamhuri ambao ni polisi na ndugu wa marehemu, Jaji alisema mashahidi hao walieleza kuwa mshitakiwa alikiri kumuua mama yake baada ya mama huyo kumrushia nyundo ambayo aliikwepa.

Kisha akamfuata mama yake na rato, wakati mama yake akirudi kinyumenyume alijikwaa kwenye kabati akaanguka chini ndipo yeye akamchoma shingoni kwa nyundo.

Jaji aliendelea kusema; Patrick kwenye maelezo hayo alikiri kuwa alichukua simu ya mama yake iliyokuwa na rangi nyekundu aina ya Tecno, kisha akaitupa kwenye shimo la maji taka na aliwaongoza polisi mpaka nyumbani ambako walivikuta vitu vyote.

"Ushahidi wa shahidi wa pili ambaye ni daktari aliyeufanyia uchunguzi mwili wa marehemu, unaonyesha kifo cha marehemu kilitokana na kukabwa shingo, kukosa hewa na alikuwa na jeraha shingoni na kupelekea shingo kuvunjika,”alisema.

Hata hivyo, akichambua ushahidi huo, Jaji Mwipopo alisema daktari alisema hawezi kusema alikufa kwa kutoka damu nyingi kwa sababu mwili wa marehemu tayari ulikuwa umeshakaa muda mrefu kabla ya yeye kuufanyia uchunguzi huo.

"Msimamo wa kisheria mauaji yanapotokea kwenye mazingira ya ugomvi, nia ovu inakuwa haipo, hivyo mahakama inamtia hatiani Patrick Mmasi kwa mauaji ya bila kukusudia,” alieleza Jaji.

Alivyojitetea mahakamani

Awali katika utetezi wake, baada ya mahakama kumuona ana kesi ya kujibu, alisema mbali ya mshitakiwa kukana kuishi kwenye nyumba hiyo na mama yake lakini pia alisema hakuna shahidi aliyeieleza mahakama kuwa alimuona akimuua marehemu.

Katika utetezi wake alisema Desemba 24, 2021 alijikuta akiwa kituo cha polisi, akiteswa na kulazimishwa akubali kumuua mama yake na kudai Desemba 27,2021 akiwa kituoni, ndipo aliposikia kwa mara ya kwanza kuwa mama yake amefariki.

Pia, mshitakiwa huyo aliiambia mahakama katika utetezi wake kuwa hakuwaongoza polisi kwenda nyumbani kwa mama yake wala hakuwepo wakati mwili wa marehemu unapatikana, wala nyundo, rato na simu kama ilivyodaiwa na baadhi ya mashahidi.

Hata hivyo, mahakama haikukubaliana na utetezi wake huo na kueleza kuwa upande wa mashitaka umeweza kuthibitisha shitaka la mauaji ya bila kukusudia kwa viwango vinavyokubalika kisheria.

Baada ya mahakama kumtia hatiani, Wakili wa serikali, Eunice Makala aliiomba mahakama impe Patrick adhabu kali iwe fundisho kwa watu wengine wanaojichukulia majukumu ya kuondoa uhai wa watu wengine.

Alisema marehemu alikuwa akitegemewa na watoto wawili akiwemo Patrick mwenyewe.

Kwa upande wake, Wakili Madeleka aliiomba mahakama impe mteja wake adhabu ndogo kwa kuwa hana rekodi ya uhalifu na kuwa, ombi lao ni mteja wake apewe adhabu ndogo hata ya kifungo cha miezi sita ili ajifunze na kujutia kosa alilofanya.

Baada ya uamuzi huo uliosomwa kwa zaidi ya saa mbili, Wakili Madeleka aliwaeleza waandishi wa habari nje ya mahakama kuwa hawajaridhika na uamuzi huo na wanatarajia kukata rufaa na Januari 10, 2024 aliwasilisha mahakamani kusudio hilo.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live