Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wakili Kibatala anusa jambo namba ya shahidi askari Polisi

Mke Wa Marehemu Bilionea Erasto Msuya, Miriam Mrita Wakili Kibatala anusa jambo namba ya shahidi askari Polisi

Wed, 6 Sep 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wakili wa mshtakiwa wa kwanza katika kesi ya mauaji ya Aneth Elisaria Msuya; Peter Kibatala amenusa jambo katika namba ya utambulisho wa askari Polisi aliyeorodheshwa katika orodha ya mashahidi wa kesi hiyo kutokana na kutofautiana kwa namba hizo.

Wakili Kibatala ameibua mkanganyiko huo wa namba za utambulisho wa askari Polisi wakati akimhoji shahidi wa 23 wa upande wa mshtaka katika kesi hiyo, WP (Polisi wa kike) Sajenti Mwaka, leo Jumanne Agosti 5, 2023.

Aneth aliyekuwa mdogo wa aliyekuwa mfanyabiashara tajiri maarufu wa madini mkoani Arusha, marehemu Erasto Msuya, maarufu kama Bilionea Msuya. Yeye Aneth aliuawa Mei 26, 2016 kwa kuchinjwa nyumbani kwake Kibada, Kigamboni, wilayani Temeke (wakati huo), jijini Dar es Salaam.

Washtakiwa katika kesi hiyo namba 103 /2018 ni Miriam Steven Mrita, mjane wa Bilionea Msuya, aliyeuawa kwa kupigwa risasi eneo la Mijohoroni, wilayani Hai mkoani Kilimanjaro Agosti 7, 2013; na mwenzake Revocatus Everist Muyella maarufu Ray.

Kesi hiyo inayosikilizwa na Jaji Edwin Kakolaki, Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, leo imeendelea kupokea ushahidi wa upande wa mashtaka kutoka kwa shahidi huyo wa 23 aliyejitambulisha kama WP 5412 Koplo Mwaka, kutoka Polisi Waya ya Kigamboni.

Katika ushahidi wake leo akiongozwa na mwendesha mashtaka, Wakili wa Serikali, Marietha Maguta, pamoja na mambo mengine, shahidi huyo ameieleza mahakama kuwa wakati wa mauaji hayo alikuwa akifanya kazi Polisi, Wilaya ya Kigamboni akiwa na cheo cha Koplo, akiwa mtunza vielelezo tangu mwaka 2011.

Kwa mujibu wa ushahidi wake, Mei 26, 2016 majira ya Mchana akiwa ofisini alipokea vielelezo vitatu kutoka kwa Sajenti John Bernard.

Vielelezo hivyo vilikuwa kwenye bahasha ndogo ya Forensic (Kitengo cha Polisi Cha Uchunguzi wa Kisayansi) vilikuwa vimeandikwa herufi kwa kila bahasha na kitu husika ndani ya bahasha yake.

"Bahasha ya kwanza iliandikwa herufi A ambayo ilikuwa ni kisu, ya pili herufi B ambayo ni chupi na bahasha ya tatu ilikuwa ni herufi C ambayo ni filimbi," amesema Sajenti Mwaka na kuongeza kuwa alifanya taratibu za kuvisajili kisha akavitunza.

Kwa mujibu kumbukumbu za mahakama zilizotokana na ushahidi wa baadhi ya mashahidi waliotangulia, kisu, chupi na filimbi ni vielelezo vilivyopatikana eneo la tukio la mauaji hayo, chumbani mwa marehemu kando ya mwili wake ulipokuwa umelala.

Shahidi huyo ameeleza kuwa alivitunza vielelezo hivyo kwenye chumba cha vielelezo mpaka Agosti 28, 2016 asubuhi, alipomkabidhi tena Sajenti Bernard, aliyekwenda kuvichukua kwa ajili ya kuvipeleka kwa mtaalam (kwa uchunguzi zaidi), baada ya kumsainisha kwenye kitabu cha vielelezo.

Baada ya maelezo hayo ya ushahidi wake wa msingi ndipo Wakili Kibatala alipomhoji pamoja na mambo mengine kama anamfahamu WP 2829 Koplo Mwaka, wa Polisi Kigamboni aliyetajwa kama miongoni mwa mashahidi wa Jamhuri, naye akakana kuwa hamfahamu.

Ifuatayo ni sehemu ya mahojiano hayo baina ya Wakili Kibatala na shahidi huyo.

Wakili Kibatala: Shahidi Unaifahamu committal (Mwenendo wa shauri la jinai wakati wa kufungwa katika mahakama ya chini lililofunguliwa kukamilisha taratibu za awali ikiwemo kukamilisha upelelezi na kuhamishiwa Mahakama Kuu kusikilizwa na kuamuriwa)?

Shahidi: Siifahamu.

Kiibatala: Ni zoezi fulani huwa linafanyika huko mahakama ya chini kabla ya kuhamishwa Mahakama Kuu na huwa tunatajiana namba za Polisi. Unamfahamu WP 2928 Koplo Mwaka Kigamboni namba 0688127395

Shahidi: Simfahamu

Kibatala: Kwa hiyo wewe namba zako ni ngapi?

Shahidi: 5412

Katika hatua hiyo upande wa mashtaka hutaja idadi na majina ya mashahidi wanaotarajiwa kuitwa kutoa ushahidi katika kesi hiyo pamoja na vielelezo utakavyoviwasilisha na kisha humsomea mshtakiwa maelezo ya mashahidi hao.

Hakuna shahidi anayeweza kutoa ushahidi kama maelezo yake hayakuwahi kusomwa katika hatua hiyo au kuorodheshwa/kutajwa na kama upande wa mashtaka utahitaki kumuita shahidi ambaye hakukidhi matakwa hayo ya kisheria unalazimika kutoa notisi mahakamani.

Namba za askari Polisi ni utambulisho wa askari husika na kila namba ni ya kipekee nchini kote hata kama majina yanafanana, na haiwezi kubadilika hata kama askari huyo cheo na wadhifa vikibadilika kwa kupanda cheo au wadhifa.

Kibatala: Shahidi ni muhimu kufuata sheria au si muhimu?

Shahidi: Ni muhimu

Kibatala: Nimesikia hapa unataka utaratibu wa kupokea vielelezo, huo utaratibu ni muhimu kuufuata?

Shahidi: Ni muhimu

Kibatala: Nimesikia umetaja kitabu cha vielelezo na hii kazi yake ni kuonesha kwa ufupi ni chain of custody (mnyororo wa utunzaji vielelezo) si ndio?

Shahidi: Ndio

Kibatala: Sasa umeeleza hapa Mei 26, 2016 ulipokea vielelezo kwa Sajenti John, bila shaka taratibu zote za kukabidhiana tunapaswa kuziona kwenye exhibit register (kitabu cha kumbukumbu ya vielelezo), si ndio?

Shahidi: Ndio.

Kibatala: Sasa umempa Jaji hicho kitabu kuonesha kwamba hivi ndivyo nilivyofanya?

Shahidi: Sijampa.

Kibatala: Ulimfafanulia Jaji kwa nini hujampa hicho kitabu?

Shahidi: Hapana sijaitoa ufafanuzi kwa sababu sikuulizwa.

Kibatala: Nilikusikia kuwa ulikabidhiwa bahasha tatu si ndio?

Shahidi: Ndio.

Kibatala: Taarifa ya kwamba bahasha A kuna kisu, B kuna chupi na C kuna filimbi ni ya kusikia ulipewa na mtu mwingine, si ndio?

Shahidi: Sajenti John aliandika kwenye bahasha.

Kibatala: Bila shaka wewe hukushuhudia wakati anaandika kwenye hizo bahasha?

Shahidi: Ndio.

Kibatala: Bila shaka mpaka leo huna uhakika na vilivyokuwemo ndani

Shahidi: Ndio, sijawahi kuviona.

Kibatala: Na ulisema tarehe 28/8/2016 ulimkabidhi tena Sajenti John, si ndio?

Shahidi: Ndio.

Kibatala: Bila shaka rekodi za kukabidhiana pia tutaziona kwenye exhibit register si ndio?

Shahidi: Hapana si lazima kwenda huko, chain of custody ni mimi kumkabidhi na yeye kupokea.

Kibatala: Ahaa sasa mwambie Jaji kwa nini ilikuwa ni muhimu kuandika wakati unapokea hivyo vielelezo?

Shahidi: Ni mujimu kuandika ili kuweka kumbukumbu endapo mimi nikifa.

Kibatala: Shahidi nani ambaye ni mtunza funguo za stoo ya vielelezo?

Shahidi: Mtunza funguo ni mimi.

Kibatala: Ndivyo mnavyofanya Kigamboni?

Shahidi: Ndio.

Kibatala: Ndivyo huwa mnafanya siku zote?

Shahidi: Hapana, ni wakati tu nilipokuwa na majukumu hayo (kutunza funguo).

Baada ya maswali hayo ya dodoso, mwendesha mashtaka alimuuliza tena shahidi huyo maswali ya kumuongoza kutoa ufafanuzi ili kusawazisha hoja zilizoibuliwa wakati wa maswali ya dodoso.

Wakili Maguta: Shahidi umeulizwa maswali mengi kuhusu vielelezo ulivyopokea kama ulivifungua na kama ulijua kilichomo, hebu ifafanulie mahakama.

Shahidi: Nilipokea vielelezo ambavyo juu ya bahasha vilikuwa vimeandikwa herufi A kisu, B chupi na C filimbi na juu ya bahasha hiyo iliandikwa IR namba 2849

Wakili: Pia Wakili alikuuliza kwenye committal iliandikwa WP 2829 na wewe ni WP 5412, hebu eleza tofauti hiyo na uhusika wako hapa.

Shahidi: Mimi ni WP 5412 huyo WP mwingine Simfahamu.

Wakili: Sasa ieleze Mahakama kuhusu vielelezo ulivyopokea tarehe 26/5/2016

Shahidi: Tarehe 26/5/2016 mimi nilikuwa mtunza vielelezo wa Polisi Wilaya ya Kigamboni na ndiye nilipokea vielelezo kutoka kwa Sajenti John Bernard.

Awali shahidi wa 22, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP), David Paulo Mhanaya, alihitimisha ushahidi wake baada ya kusimama kizimbani kwa siku nne; kwa kutoa ufafanuzi wa mambo mbalimbali yaliyoibuliwa na mawakili wa utetezi wakati wa maswali ya dodoso waliyomhoji.

Shahidi huyo alikuwa ndiye mpelelezi mkuu wa kesi hiyo ambaye kwa kiongozwa na mwendesha mashtaka Wakili wa Serikali Mwandamizi, Paul Kimweri, ambaye alikuuliza maswali.

SSP Mhanaya alikuwa kiongozi wa timu ya upelelezi wa mauaji hayo iliyoteuliwa na aliyekuwa Mkurugenzi wa Upelelezi wa Mkosa ya Jinai (DCI) wakati huo, Diwani Athumani Msuya, baada ya kutoridhishwa na jinai upelelezi wa awali ulivyokuwa ukiendelea.

Kwa Sasa SSP Mhanaya ni Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai mkoa wa Arusha (RCO)

Wakili Kimweri: Shahidi nitakuhoji maswali kutokana na yale ambayo uliulizwa. Uliulizwa kuhusu kielelezo cha 16 cha upande wa mashtaka (hati ya upekuzi), kama kuna PF (fomu ya Polisi) namba hebu ieleze Mahakama.

Shahidi: Mheshimiwa Jaji hii ni hati ya dharura ya ukamataji mali kwa mtuhumiwa na huwa haina namba. Unaweza ukaandika pale unapomkamata mtuhumiwa

Wakili: Uliulizwa pia swali kuwa umeandika humo eneo la Olasiti lakini ukaambiwa hakuna neno Arusha, ifafanulie mahakama.

Shahidi: Mheshimiwa Jaji ni kweli sikuandika neno Arusha kwa sababu kama nilivyosema niliondoka kwenda Arusha kumkamata mtuhumiwa. Kwa kuwa nilishaeleza nilikwenda Arusha, na kwa kuwa nilimkamata eneo la Olasiti Kata ya Burka sikuona haja ya kuandika neno Arusha.

Wakili: Uliulizwa pia kuhusiana na majina Revocatus Everist Mollel aka Ray ukaambiwa yanatofautiana na mshtakiwa (majina ya mshtakiwa wa pili) Revocatus Everist Muyella, hebu ifafanulie mahakama.

Shahidi: Mheshimiwa Jaji ni kweli mtuhumiwa anaitwa Revocatus Everist Muyella, lakini pia kuna hati yake ya kuhitimu mafunzo ya mgambo kuna majina ya Revocatus Everist Mollel a.k.a Ray. Lakini pia nilimkuta na kitabu cha bunduki cha jina Revocatus Everist P. Mollel.

Wakili: Uliulizwa pia kama ulifanyia uchunguzi jina la Revocatus Everist Mollel kama hilo jina linahusiana na mtuhumiwa, ifafanulie mahakama.

Shahidi: Mheshimiwa Jaji sikulifanyia uchunguzi kwa sababu kwanza ni nyaraka ambazo nilizikutaka kwa mtuhumiwa na hakuwa na ubishi wowote kuhusu majina hayo lakini pia ndiye aliyeweka saini kwenye hii hati ya upekuzi.

Wakili: Pia uliulizwa swali kuhusiana na jina lililo kwenye kitabu cha umiliki bastola Revocatus Everist P. Mollel kama ulifanya uchunguzi wa jina hilo kama linahusiana na mshtakiwa wa pili, hebu ifafanulie mahakama.

Shahidi: Mheshimiwa Jaji Sikufanya uchunguzi wa jina hilo kwenye kitabu hicho kwa sababu tukio lililoko hapa ni la marehemu kuchinjwa na siyo kupigwa risasi.

Wakili: Sasa kuhusiana na ushahidi wa mawasiliano ya simu ya mshtakiwa wa kwaza unalifafanuaje?

Shahidi: Mheshimiwa Jaji uchunguzi wa mawasiliano ya simu ya mtuhumiwa wa kwanza haikuwa na uhusiano na tukio hili kwani kama nilivyoeleza mtuhumiwa alitumia simu nyingine kama, watakavyokuja kueleza wataalamu wa mawasiliano.

Wakili: Shahidi uliulizwa swali kama ulipata kujua namba za simu ambayo Getruda alipewa, katika hili unasemaje?

Shahidi: Mheshimiwa Jaji simu ya Getruda hatukuweza kuipata kwani alikuwa ameshaitupa kama alivyoeleza, hivyo hatukuifanyia uchunguzi kwani huwezi kufanyia uchunguzi wakati huna hata simu card.

Wakili: Uliulizwa pia kuhusiana na mume wa marehemu Aneth kwamba aliwahi kuwa na mgogoro, ukaulizwa kama uliwahi kutoa amri ahojiwe, hebu ifafanulie mahakama.

Shahidi: Mheshimiwa Jaji ni kweli nilitoa maelekezo mume wa Aneth Wilbroad (usahihi Wilbard ) Kimaro ahojiwe kubaini hizo allegation (tuhuma) kuwa alikuwa na mgogoro na marehemu, lakini haikuthibitika kuwa na mgogoro na hakuwa na connection (muunganiko) na tukio hili la mauaji.

Wakili: Shahidi ulioneshwa hii document hebu ifafanulie mahakama ni kitu gani?

Shahidi: Mheshimiwa Jaji hii ni first crime report kwa maana ni taarifa za Polisi za ndani ambazo zinatoa taarifa za awali jinsi tukio lililvyotokea. Haina maana kwamba ndio zinaweza ku-conclude kuwa unaweza ukamchukua mtu huyu mpaka, zifanyiwe uchunguzi wa kina.

Wakili: Hebu itajie mahakama hao suspect (watuhumiwa) waliotajwa kwenye hiyo document.

Shahidi: Mheshimiwa Jaji suspect ambao wametajwa awali ni Getruda Peniel Mfuru (aliyekuwa mfanyakazi wa ndani wa marehemu Aneth), Sabri Haji Kombo (mpenzi wa Getruda), Wilbad Mathew Kimaro (aliyekuwa mume wa marehemu Aneth - waliyekuwa wametengana), Twaha Almas na Amir Almas Said.

Wakili: Uliulizwa ni lini walikamatwa, hebu ielezee mahakama.

Shahidi: Kwa mujibu wa hii photocopy (nakala kivuli ya taarifa hiyo ya awali) ni tarehe 27/5/2016. Lakini sahamani Mheshimiwa Jaji hapohapo kuna kitu ambacho kinaleta mashaka. Kuna tarehe hapo chini iliyoandikwa hii document tarehe 11/7/2016. Kwa hiyo hii inaleta mashaka.

Mheshimiwa Jaji hizi first crime report inaandaliwa immidieltly tukio linapokaguliwa. Kwa hiyo hii tu hapa ina mashaka kwamba ripoti hii imeandaliwa kimagumashi

Wakili: Sasa hebu ifafanulie mahakama kuwa hao watuhumiwa waliotajwa hapo walikamatwa tarehe hiyo.

Shahidi: Mheshimiwa Jaji inaweza kuwa hakuna ubishi lakini bahati document hii ina mashaka kwani tarehe zimeshagongana. Na hapa inaonesha uchunguzi ulikuwa bado unaendelea na kwamba tukio lilifanywa na watu wasiojulikana.

Mheshimiwa Jaji taarifa hii inaonesha kuwa bado ni uchunguzi wa awali. Kwa hiyo hata hawa waliotajwa wanaweza kuwa hawana maana ndio maana hata Getruda alipopatikana baada ya kumhoji niliona si mtuhumiwa. Baadaye uchunguzi uliingia deep (ulifanyika kwa kina) ndio maana hawa washtakiwa wako hapa mahakamani.

Wakili: Umeulizwa pia kuhusiana na postmortem report (taarifa ya uchunguzi wa kitabibu kuhusu sababu za kifo) kuhusu marehemu Aneth alifariki muda gani, hebu ifafanulie mahakama.

Shahidi: Mheshimiwa Jaji hapa muda muda wa saa 24. Hakuna muda maalum.

Wakili: Uliulizwa pia umbali kutoka nyumba ya Aneth mpaka nyingine ukajibu kuwa ni kama mita 15 ifafanulie mahakama.

Shahidi: Nyumba ya Aneth ilikuwa fenced (imezungushiwa ukuta) na ilikuwa umbali wa mita 15 kwa sababu hizo hakukuwa na uwezekano watu wengine kujua kilichokuwa kinaendelea ndani ya nyumba ile.

Wakili: Uliulizwa pia kuhusiana na ushahidi wa sumu kuhusika katika tukio hili, hebu ifafanulie mahakama kuhusu hilo.

Shahidi: Mheshimiwa Jaji katika kesi hii tangu nilipopeleleza sijapata hoja kuhusiana na sumu bali marehemu aliuawa kwa kuchinjwa.

Wakili: Uliulizwa pia kuwa baada ya tukio hili Getruda alikuwepo na hakutoa ripoti hebu fafanua majibu uliyatoa.

Shahidi: Mheshimiwa Jaji, Getruda aliondoka kabla ya tukio hili kwenda kwa mpenzi wake Sabri Kombo. Hilo litakuja kuthibitishwa na shahidi mwenyewe Getuda na Sabri Kombo.

Wakili: Uliulizwa kama ulithibitisha kuwa Geteuda alipewa nauli (na mpenzi wake kwenda kwao baada ya tukio).

Shahidi: Mheshimiwa Jaji ni kweli Geteuda alipewa nauli na Sabri Kombo na yeye mwenyewe atakuja kuthibitisha hilo.

Wakili: Uliulizwa pia kama uliwahoji mashahidi majirani wa Aneth, ulijibu nini na fafanua majibu hayo.

Shahidi: Niliwahoji Mheshimiwa Jaji na hakukuwa na mtu aliyesema Aneth alikuwa na ugomvi na mtu yeyote katika eneo hilo.

Wakili: Uliulizwa kama ulimhoji mtoto wa Aneth (Allan) hebu fafanua;

Shahidi: Hatukuona haja kumhoji kwa sababu inaonekana hata uelewa wake ulikuw ni mdogo kama shahidi mama muuza vitumbua alivyoeleza kwamba alikwenda kumwambia kuwa mama yake amelala na haamki halafu amechafuka. Kwa hiyo inaonesha hata hakujua kama amekufa.

Wakili: Vilevile uliulizwa kuhusu mahali mwili wa Aneth ulikutwa, hebu ifafanulie mahakama.

Shahidi: Mheshimiwa Jaji kama nilivyosema awali tulipokwenda eneo la tukio tarehe 12/6/2016, timu nyingine ilikuwa imeshafanya uchunguzi hivyo vitu vingi havikuwa katika uhalisia.

Wakili: Uliulizwa kuhusu De France hotel kuwa hakukuwa na footage kuonesha kama mtuhumiwa Miriam alifikia hapo, hebu ifafanulie mahakama.

Shahidi: Ni kweli lakini mhalifu kama anapanga uhalifu hata gari anaweza akaficha sehamu nyingine.

Wakili: Uliulizwa pia kuhusiana na usajili na kuhamisha umiliki wa magari T800CKF, hebu ifafanulie mahakama.

Shahidi: Mheshimiwa Jaji kuhusu umiliki wa magari T800CKF Rangerover na T677BNM Toyota Landcruiser, ni kwamba magari haya mawili hayana connection na kesi hii, haya tulichukua kadi zake kwa uchunguzi na si gari na hayahusiani na tukio hili.

Wakili: Uliulizwa pia kuhusu kesi ya mirathi kwamba ndugu wa Msuya walipewa mirathi, unasemaje katika hilo?

Shahidi: Mheshimiwa Jaji kesi hiyo ya mirathi haihusiani na kesi hii ya mauaji.

Wakili: Uliulizwa kama ulizingatia kifungu cha 33 CPA (Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai) kama ulizingatia masharti yake, ifafanulie mahakama.

Shahidi: Mheshimiwa Jaji kifungu cha 33 hakinihusu mimi, kinamhusu mkuu wa kituo (OCS), mimi sikuwa mkuu wa kituo, nilikwenda (katika Kituo Kikuu cha Polisi baada ya kuwakamata watuhumiwa) kama mpelelezi

Wakili: Uliulizwa pia kuhusu masharti ya kifungu cha 38 kama ulitoa risiti hebu ifafanulie mahakama.

Shahidi: Suala la kutoa risiti mimi baada ya upekuzi nilitoa certificate of seizure (hati ya ukamataji mali), hii ndio inatumika kama risiti hata ukienda Polisi kokote Tanzania suala la risiti halipo.

Wakili: Uliulizwa kuhusu kitabu cha kumiliki silaha (kwa mshtakiwa wa pili) na nakala ya hati ya mafunzo ya mgambo kwamba kwa nini hukuvileta mahakamani, hebu ifafanulie mahakama.

Shahidi: Mheshimiwa Jaji sikuona umuhimu wa kuvileta kwa sababu havihusiani na kesi hii.

Wakili: Uliulizwa pia vitu ambavyo ulivihodhi kutoka kwa mshtakiwa wa kwanza (mikufu na nguo) kwamba hujavileta, ifafanulie mahakama hilo.

Shahidi: Mheshimiwa Jaji vitu ambavyo havijaletwa hapa kwa sababu havihusiani na kesi hii ndio maana Jamhuri hawajaniambia nivilete.

Wakili: Wakili Nkoko pia alikuonesha statement ile ambayo uliandika akasema kuna mambo uliyaeleza hapa mahakamani na.kwenye statement hayapo, unaieleza nini Mahakama?

Shahidi: Mheshimiwa Jaji kwanza kwenye statement yangu hakuna mgongano wowote. Lakini pia hakuna sheria inayonizuia kueleza kile.ambacbo nimekikumbuka ambacho hakiko kwenye statement. Lakini maelezo yangu yote ni sahihi na kwenye statement yangu nimeeleza summary (muhtasari) tu.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live