Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wakazi Dar kortini kilo 51 za heroine

8c95ba89d791587c9ec0b619b9575053 Wakazi Dar kortini kilo 51 za heroine

Thu, 17 Sep 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

WAKAZI wanne wa Dar es Salaam, wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashitaka matatu likiwemo la kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya aina ya heroine zenye uzito wa kilogramu 51.47.

Washitakiwa hao ni Ernest Semayoga Mkazi wa Mbezi Beach A, Salum Jongo (45) mkazi wa Mbezi Beach A, Amini Sekibo (25) na Tatu Nassoro (45) Mkazi wa Temeke.

Akisoma mashitaka hayo mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Kasian Matembele.

, Wakili wa Serikali Mkuu, Paul Kadushi akisaidiana na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon na Wakili wa Serikali, Benson Mwaitenda, alidai washitakiwa walijihusisha na biashara haramu ya dawa za kulevya, utakatishaji fedha na kuongoza genge la uhalifu.

Kadushi alidai katika mashitaka ya kwanza kuwa Septemba 8 mwaka huu maeneo ya mtaa wa Vetenari wilayani Temeke, Dar es Salaam, washitakiwa kwa pamoja walijihusisha na biashara haramu ya dawa za kulevya zenye uzito wa kilogramu 51.47 aina ya heroine.

Katika shitaka la pili ilidaiwa kuwa, kati ya Septemba Mosi na 8 mwaka huu maeneo ya ndani na nje ya jiji la Dar es Salaam, washitakiwa walijipatia Sh 62,970,000, fedha za Msumbiji 7,370, shilingi za Kenya 400, magari manane, kompyuta mpakato aina ya Apple, shamba la ekari 19 lililopo Fukayosi Bagamoyo mkoani Pwani na nyumba mbili Mbezi Beach wakati wakijua mali hizo zilitokana na usafirishaji wa dawa za kulevya.

Katika shitaka la tatu, Simon alidai kati ya Septemba Mosi na 8 mwaka huu katika maeneo tofauti ya ndani na nje ya jiji la Dar es Salaam, washitakiwa waliongoza genge la uhalifu kwa kujihusisha na biashara haramu ya dawa za kulevya zenye uzito wa kilogramu 51.47 aina ya heroine.

Washitakiwa hawakutakiwa kujibu chochote kwa sababu Mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi za uhujumu uchumimpaka itakapopata kibali kutoka kwa Mkurugenzi wa Mashitaka nchini (DPP).

Wakili Kadushi alidai sehemu kubwa ya upelelezi umefanyika na kwamba wanaratibu kukamilisha sehemu ya upelelezi uliyobaki hivyo, waliomba tarehe nyingine kwa ajili ya kukamilisha taratibu za kupeleka mashitaka hayo Mahakama Kuu.

Hakimu Matembele aliahirisha kesi hiyo hadi Septemba 30 mwaka huu kwa ajili ya kutajwa na washitakiwa walirudishwa rumande kwa sababu mashitaka yanayowakabili hayana dhamana kisheria.

Chanzo: habarileo.co.tz