Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wakataa wanaume kuwapekua wanawake mgodi wa Tanzanite

10092 Madini+pic TZW

Tue, 26 Jun 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mirerani. Wakazi wa Mji mdogo wa Mirerani wilayani Simanjiro mkoani Manyara, wameiomba Serikali kuweka utaratibu mzuri wa kuingia ndani ya ukuta unaozunguka migodi ya madini ya Tanzanite ikiwemo wanawake kutowapekua wanaume na lango la kuingia liwe wazi kwa saa 24.

Wakizungumza leo Juni 26, wakazi hao wameiomba Wizara ya Madini, kujipanga upya na kuweka mfumo mpya utakaowawezesha kuingia ndani ya ukuta huo tofauti na ilivyo sasa. 

Dereva wa pikipiki ya kubebea abiria (bodaboda) wa mji mdogo wa Mirerani, Rashid Hamis amedai kuwa wanapata wakati mgumu wanapotaka kutoka ndani ya ukuta huo, pindi wanapopekuliwa mfukoni. 

Rashid alisema askari polisi wa kike wa eneo hilo huwa wanawapekua mifukoni na kuwashika sehemu za siri na kuwasababishia mfadhaiko hivyo utaratibu huo ubadilishwe. 

Mwenyekiti wa kijiji cha Naisinyai, Taiko Kurian amesema utaratibu wa kufunga lango la kuingia ndani ya ukuta unaozunguka migodi hiyo kila ifikapo saa 5 usiku si mzuri, unawakwaza wengi. 

Taiko alisema ingepaswa lango hilo kuwa wazi kwa saa 24 ili endapo kukitokea tatizo liweze kupata msaada ikiwemo ajali au dharura zozote zinazoweza kutokea mgodini kwani shughuli za machimbo hufanyika mchana na usiku. 

Mwenyekiti wa chama cha wachimbaji madini wa Mkoa wa Manyara, Sadiki Mneney alisema jitihada za ofisa madini mkazi wa Mirerani Daudi Ntalima zinaonekana katika kutumikia nafasi hiyo. 

Mneney amesema mfumo wa Ntalima kukutana na wadau wa madini na kuwasikiliza matatizo yao na kero zao aliouanzisha unapaswa kuendelezwa kwani unaonekana una mafanikio kwa wadau. 

Hata hivyo, Ofisa Madini mkazi wa Mirerani, Daudi Ntalima alisema suala la kupekuliwa itabidi liendelee hivyo hadi hapo mfumo wa kamera na vyombo vya kisasa vya upekuzi vitakapowekwa ndipo utaratibu huo utafikia mwisho. 

"Kwa upande wa lango kufungwa saa 5 usiku si tatizo kwani mameneja wa migodi wana namba za simu za watu wote wanaohusika hivyo kukiwa na dharura huwa linafunguliwa wakati wowote ila baadaye litakuwa wazi kwa saa 24," amesema Ntalima. 

 

Chanzo: mwananchi.co.tz