Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wakala wa Manispaa apandishwa kortini kwa kughushi hati

16010 Wakala+pic TanzaniaWeb

Fri, 7 Sep 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar Es Salaam. Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), imempandisha kizimbani, Wakala wa Manispaa ya Arusha, Robert Modu, kujibu mashtaka matatu likiwemo la kujipatia Sh23milioni kwa njia ya udanganyifu, mali ya Kampuni ya Sigara Tanzania (TCC).

 Hata hivyo hati ya mashtaka haikueleza, Modu ni wakala anayesimamia eneo gani, manispaa ya Arusha.

Modu ambaye, pia ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Robert Advertisements Ltd, amepandishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na kusomewa mashtaka yake, mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi Wanjah Hamza.

Wakili kutoka Takukuru, Leonard Swai alidai kuwa mshtakiwa anadaiwa kutenda makosa yake kati ya Desemba 4, 2013 na Julai 14, 2014 katika eneo la Kijitonyama, wilaya ya Kinondoni.

Katika shtaka la kwanza, inadaiwa kuwa kwa nia ovu, Modu alitengeneza hati ya madai ya uongo yenye kumbu kumbu namba RA/CC &ADV/VOL.1/1078, akidai  kuwa hati hiyo imetolewa na Manispaa ya Jiji la Arusha, wakati akijua sio kweli.

Swai alidai katika shtaka la pili, siku na tarehe hizo, Modu akiwa katika  ofisi za kampuni ya Sigara Tanzania iliyopo Manispaa ya Ilala,  aliwasilisha hati ya madai ya uongo yenye kumbu kumbu namba RA/BB&ADV/VOL.1/1078, akionyesha kuwa hati hiyo imetolewa na Manispaa ya Jiji la Arusha, wakati akijua kuwa sio kweli.

Iliendelea kudaiwa Mahakamani hapo kuwa, kati ya Novemba 4, 2013 na Julai 14, 2014 katika kampuni ya Sigara, iliyopo Ilala, akiwa wakala wa Manispaa ya Mji wa Arusha alijipatia Sh23 milioni kwa njia ya udanganyifu, akidai kuwa kiasi hicho kimeidhinishwa na Jiji la Arusha na yeye alizipokea kwa niaba ya Manispaa ya Arusha.

Mshtakiwa alikana mashtaka yanayomkabili na Swai alidai kuwa upelelezi shauri hilo umekamilika hiyo wanaomba terehe nyingine kwa ajili ya kumsomea maelezo ya awali mshtakiwa.

Hakimu Hamza aliyataja masharti ya dhamana kuwa ni mshtakiwa kuwa na wadhamini wawili wataosaini bondi ya Sh 10milioni au kuwasilisha hati ya mali isiyohamishika yenye kiasi hicho cha Fedha.

Chanzo: mwananchi.co.tz