Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wakacha kifungo cha miaka 20 jela baada ya kulipa faini

Wed, 28 Aug 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Watu sita wamekwepa kutumikia kifungo cha miaka 20 jela baada ya kulipa faini ya Sh125 milioni.

Washtakiwa hao walihukumiwa leo Jumanne Agosti 27, 2019 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Pia wametakiwa kulipa fidia zaidi ya Sh216.5 milioni  huku mahakama ikitaifisha Sh42 milioni  na fedha ya Rwanda franc 75,000.

Washitakiwa hao ni Faisal Ally (31), Isack Shija (28), Abdulkarimu Doshi (25), Abas Said (23), Nassoro Sleyyum na Ahmed Abubakari (32).

Hukumu hiyo imesomwa na Hakimu Mkazi, Janeth Mtega baada ya washtakiwa hao kukiri kosa kutokana na kutiwa hatiani kwa makosa matano  ikiwemo kusafirisha madini ya Sh2.9 bilioni.

Hakimu Mtenga amesema washtakiwa kwa pamoja  walishiriki genge la uhalifu, kusafirisha madini nje ya nchi, kuuza madini kinyume na sheria, kushindwa kulipa mrabaha na kuisababishia hasara Serikali.

Amesema katika shtaka la kwanza kila mshtakiwa anatakiwa kulipa faini ya Sh5 milioni au kwenda jela miaka 20, shtaka la pili wote kwa pamoja wanatakiwa kulipa faini ya Sh5 milioni au kwenda jela mwaka mmoja

Katika shtaka la tatu la kuuza madini kinyume na sheria kwa pamoja wanatakiwa kulipa faini ya Sh5 milioni au kwenda jela mwaka mmoja na shtaka la nne linalomkabili  Ally la kushindwa kulipa mrabaha zaidi ya Sh216.5 milioni,  alitakiwa kulipa faini ya Sh5 milioni au kwenda jela mwaka mmoja.

Shtaka la tano washtakiwa wote wamehukumiwa kulipa faini ya Sh5 milioni au kwenda jela miaka 20 baada ya kuisababishia hasara Serikali zaidi ya Sh216.5 milioni.

Hakimu Mtega amesema washtakiwa wakishindwa kulipa faini kila mmoja atatumikia kifungo cha miaka 20 jela.

Hata hivyo wote walilipa faini na kukwepa kifungo.

Kabla ya kutoa adhabu hiyo Wakili wa Serikali mwandamizi, Wankyo Simon amedai kesi hiyo ilikuja kwa ajili ya kutajwa na upelelezi umekamilika.

Washtakiwa hao baada ya kusomewa maelezo walikiri makosa yao.

Chanzo: mwananchi.co.tz