Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wahukumiwa kulipa Sh26.4 milioni baada ya kuisababishia hasara Serikali

Wahukumiwa kulipa Sh26.4 milioni baada ya kuisababishia hasara Serikali

Thu, 31 Oct 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Watu watano akiwamo wakala wa Kampuni ya mtandao wa simu Tigo, Hamis  Singa wamehukumiwa kulipa fidia ya Sh26.4  milioni baada ya kuisababishia hasara Serikali kwa kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.

Pia, Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imewahukumu kulipa faini ya Sh300, 000 kila mmoja  na wakishindwa watumikie kifungo cha miaka Saba gerezani kwa kosa la kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu kupitia ujumbe mfupi mitandaoni.

Mbali na Singa wengine waliohukumiwa ni Jailos Joseph,  Singa Elisha, Japhet Mkumbo na Omari Omari .

Akisoma hukumu hiyo leo Jumatano Oktoba 30, 2019, Hakimu Mkazi Mkuu, Salum Ally amesema Mahakama hiyo imeamuru vifaa ambavyo walikuwa wakivitumia washtakiwa hao  kufanyia utapeli ambavyo ni simu 11, laini za simu mbali mbali 11, gramu 6.8 za madini feki ya Tanzanite na mizani wa kupimia madini vitaifishwe kuwa mali ya Serikali

Ally amesema kwa kuwa washitakiwa hao  wamefanya makubaliano na Mkurugenzi wa Mashitaka nchini (DPP), adhabu ya faini  ni ya kwanza ili iwe fundisho kwa wengine. Amesema washtakiwa wanatakiwa kulipa pia faini ya Sh300,000 kila mmoja au kutumikia kifungo cha miaka saba gerezani. “Makubaliano mliyoingia na DPP  yatekelezeke kwa kufidia hasara mliyosababisha hivyo mnatakiwa kulipa fidia ya Sh26,432,441 milioni,” amesema.

Kabla ya kutolewa kwa adhabu hiyo, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Renatus Mkude alidai hawana kumbukumbu ya makosa ya nyuma ya washtakiwa na kuomba mahakama izingatie makubaliano waliyoingia. Alisema katika makubaliano hayo washtakiwa watalipa fidia ya Sh26.4 milioni na kutaifisha vitu vyote walivyokamatwa navyo.

Katika utetezi wao, washitakiwa hao waliomba mahakama hiyo iwape adhabu ya kulipa faini kwani wao ni wakosaji wa kwanza pia wanafamilia zinazowategemea, aidha ni vijana ambao ni nguvu kazi wa kesho na pia bado wanamzigo mkubwa wa kulipa fidia kama walivyokubaliana na DPP.

Washtakiwa hao wanadaiwa, kati ya Januari na Julai 2019 katika mikoa ya Manyara, Arusha na mikoa mingine nchini kwa njia ya udanganyifu walijipatia Shilingi 26,432,441 kwa kusambaza ujumbe au taarifa isemayo ile fedha tuma kwenye namba hii huku wakijua kuwa ujumbe huo ni wa uongo na una lengo la kupotosha umma.

Chanzo: mwananchi.co.tz