Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wahitimu darasa la 7 wahujumu shule

D177b102109cf5e5e08178c806f981d3 Wahitimu darasa la 7 wahujumu shule

Wed, 14 Oct 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

WAHITIMU wanane wa darasa la saba katika shule ya awali na msingi ya Kibaha Independent (KIPS),wakati wakisubiri wazazi wao kuwachukua baada ya kumaliza mitihani, wamefanya vurugu na kusababisha hasara kubwa.

Kutokana na vurugu hizo uongozi wa shule hiyo umewataka wazazi wa watoto hao kufika shuleni hapo kuona uharibifu uliofanywa na watoto wao na kujadiliana namna ya kufanya.

Akizungumza kwenye mahafali ya 15 ya shule hiyo, Mwenyekiti wa bodi ya shule hiyo, Yusufu Mfinanga alisema wazazi wa wahitimu hao wanapaswa kuonana na uongozi wa shule kujadili suala hilo.

"Wahitimu hawa walifanya vurugu baada ya kumaliza mitihani na walikuwa wakiwasubiri wazazi wao ili kurudi majumbani," alisema.

Wanafunzi hao walipasua vioo, feni na baadhi ya vifaa vya umeme kwenye shule hiyo na endapo hatua za haraka zisingechukuliwa wangeweza kuleta madhara makubwa zaidi.

"Kutokana na uharibifu huu, wazazi wa wanafunzi hawa wanapaswa kutoa ushirikiano kwa uongozi wa shule ili kulimaliza suala hili na endapo watashindwa kutoa ushirikiano hatua za kisheria zitachukuliwa," alisema.

Mgeni rasmi kwenye mahafali hayo ambaye pia ni Mkurugenzi wa Shirika la Elimu Kibaha, Robert Shilingi alisema elimu waliyoipata ni msingi tu kwani ulimwengu wa sasa unahitaji wahitimu wasomi wenye elimu na upeo wa juu.

Shilingi alisema endapo wahitimu wa ngazi mbalimbali watakuwa na elimu kubwa wataweza kutumia changamoto kuwa fursa ili kujikwamua na hali ngumu na kujikuta wakijiajiri, badala ya kusubiri kuajiriwa.

Meneja wa shule hiyo, Nuru Mfinanga alisema ili shule na wanafunzi waweze kufanya vizuri wazazi wanapaswa kutoa ushirikiano kwa kulipa ada kwa wakati.

Kwa upande wake mwakilishi wa idara ya elimu msingi ya Halmashauri ya Mjini Kibaha, Ramadhan Laoga alisema wazazi walioamua kuwekeza elimu kwa watoto wao wamefanya jambo jema kwani uwekezaji kwa watoto ni urithi ambao hauwezi kupotea.

Chanzo: habarileo.co.tz