Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wahamiaji haramu 68 wakamatwa

Wahamiaji Haramu Pic Data Wahamiaji haramu 68 wakamatwa

Mon, 21 Mar 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Jeshi la Polisi Mkoa wa Kilimanjaro kwa kushirikiana na idara ya Uhamiaji mkoani humo, limewakamata wahamiaji haramu 68 ambao wanadaiwa kuwa raia wa nchini Ethiopia na Somalia kwa kosa la kuingia nchini kinyume cha sheria.

Akitoa taarifa za kukamatwa kwa watu hao leo Jumatatu Machi 21, 2022, kaimu Kamanda wa Polisi mkoani Kilimanjaro, Yahaya Mdogo amesema wahamiaji haramu 60 ni raia wa Ethiopia ambao walikamatwa Machi 19, 2022 katika Kata ya Lembeni wilayani Mwanga huku wengine nane wakiwa ni raia wa Somali ambao walikamatwa Machi 20 katika eneo la Ngarenairobi wilayani Siha.

Mdogo amesema wahamiaji hao wenye umri kati ya miaka 18-38, walikamatwa na askari waliokuwa doria na uchunguzi unaendelea kwa kushirikiana na idara ya uhamiaji ili kubaini waliowasafirisha na njia walizotumia.

"Tumekamata raia 60 wa nchini Ethiopia katika eneo la Lembeni Mwanga na wengine nane wa Somalia ambao walikamatwa wakiwa kwenye gari katika eneo la Ngarenairobi Siha, dereva alikimbia na kulitelekeza gari, raia hawa waliingia nchini bila kibali kwa kupita njia za panya" amesema.

Kwa upande wake Mkuu wa Idara ya Uhamiaji Mkoa wa Kilimanjaro, Edward Mwenda amewataka wananchi kushirikiana na vyombo vya ulinzi, kuwabaini wahamiaji haramu wanaoingia nchini na wale wanaoshiriki kuwasafirisha.

Mwenda amesema katika mahojiano na wahamiaji haramu hao wamedai kuwa walikuwa wakipita nchini kwenda Afrika Kusini kutafuta maisha na kueleza kuwa wanaendelea na operesheni kuhakikisha Mkoa huo hauwi uchochoro wala vichaka vya kupitisha wahamiaji haramu.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live