Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wahamiaji haramu 32 wakamatwa Tanga

Wahamiaji Haramu.jpeg Wahamiaji haramu 32 wakamatwa Tanga

Wed, 30 Sep 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

J ESHI la Polisi mkoani Tanga limewakamata porini wahamiaji haramu 32 wakiwemo raia 28 wa Ethiopia na Wasomali wanne.

Awali, Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa) lilitoa taarifa kuwa askari wa Hifadhi ya Taifa Saadan wamekamata wahamiaji haramu 28 katika eneo la Bahari jirani na kijiji cha Buyuni, wilayani Pangani, mkoani Tanga.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Blasius Chatanda alisema jana kuwa wahamiaji hao walikamatwa kwenye kijiji hicho wakiwa wamejificha porini baada ya kushindwa kuendelea na safari kwa kuwa boti waliyokuwa wakisafiria ilikwama kwenye mchanga.

“Unajua kwenye bahari kina maji kupwa na maji kujaa, sasa wao walipofika eneo hilo la Buyuni maji ya bahari yalikupwa na boti ikakwama ikabidi waitelekeze boti yao na kujificha porini,” alisema Kamanda Chatanda.

Alisema, taariofa zililifikia jeshi hilo kuhusu wahamiaji hao na kwa kuwa walikuwa mbali waliwaomba walinzi wa Tanapa wakawazingira na kuwakamata.

Kamanda Chatanda alisema wahamiaji wengine wanne raia wa Somalia ambao kati yao yumo mwanamke, walikamatwa jana asubuhi na askari hao wa Tanapa na kukabidhiwa kwa jeshi hilo.

Taarifa iliyotolewa na Kamishna Msaidizi Mwandamizi Tanapa-Mawasiliano, Pascal Shelutete ilieleza kuwa Tanapa wamekamata watu 28 wanaoshukiwa kuwa ni wahamiaji haramu.

Alisema uongozi wa Hifadhi ya taifa ya Saadani tayari umewakabidhi washukiwa hao kwa Jeshi la Polisi kwa hatua zaidi za kisheria.

“Tunatoa onyo kwa wale wote wenye dhamira ya kutumia hifadhi za taifa kuwa maeneo ya kufanya vitendo ambavyo ni kinyume cha sheria na kwamba wasithubutu kufanya hivyo kwnai tumejipanga vyema,” ilieleza taarifa ya Shelutete.

Chanzo: habarileo.co.tz