Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wahamiaji haramu 20 wakamatwa Kilimanjaro Februari pekee

Mbaroni Kwa Kuwakalisha Chini Wanafunzi, Kuwapiga Picha Wahamiaji haramu 20 wakamatwa Kilimanjaro Februari pekee

Wed, 22 Feb 2023 Chanzo: mwanachidigital

Jeshi la Uhamiaji mkoa wa Kilimanjaro limeendelea na operesheni maalumu ya kukamata wahamiaji haramu wanaoingia nchini kinyume cha sheria na taratibu ambapo Februari 2023 pekee, wamewakamata zaidi ya wahamiaji haramu 20.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, mkuu wa uhamiaji mkoa wa Kilimanjaro, kamishna msaidizi wa uhamiaji, Edward Mwenda amesema wanaendelea na operesheni ya kudhibiti wahamiaji haramu kuingia nchini kinyume cha sheria na kuwataka wananchi wanaoishi maeneo ya mipakani kutoa ushirikiano.

Mwenda amesema wamekuwa wakishirikiana na vyombo vingine vya usalama kudhibiti wahamiaji haramu nchini ambapo katika kipindi cha Januari hadi Desemba 2022 walikamata wahamiaji haramu 438 kutoka mataifa mbalimbali.

“Kama mnavyoelewa mkoa wetu unapakana na nchi jirani ya Kenya, hivyo tunaendelea na udhibiti na usimamizi wa mipaka yetu ili kuhakikisha raia wa kigeni na Watanzania wanaingia na kutoka nchini kwa kufuata sheria na taratibu zilizopo.

“Kutokana na jukumu hilo, tumekuwa tukiendesha doria, misako na operesheni katika maeneo ya mipakani pamoja na kutoa elimu ili kushirikisha wananchi katika ulinzi wa mipaka yetu na kuhakikisha raia wa kigeni wanaingia nchini kwa kufuata njia rasmi ambazo kwa mkoa wa Kilimanjaro ni Kituo cha Holili na Tarakea wilayani Rombo, na kama anaingia kwa anga ni Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA).

Ameongeza kuwa: “Kufuatia operesheni hiyo, katika kipindi cha Januari hadi Desemba 2022 tuliwakamata wahamiaji haramu 438 na kati ya hao, 277 ni raia wa nchini Ethiopia na wengine ni wa mataifa mbalimbali na wote walichukuliwa hatua ikiwemo kufikishwa mahakamani na wengine kuondoshwa nchini.”

Amesema: “Lakini kwa mwezi huu kuanzia Februari Mosi hadi sasa, katika operesheni hiyo ambayo ni endelevu tumekamata raia wa kigeni kutoka mataifa mbalimbali zaidi ya 20 ambao wamekiuka sheria za uhamiaji, na operesheni hii ni endekevu, tunapenda wageni waje nchini, lakini wafuate sheria.”

Amesema wahamiaji haramu wanaingia nchini kwa malengo mbalimbali ikiwemo kufuata shughuli za kiuchumi kama kilimo na biashara, huduma za matibabu na wengine wakitaka kupita njia kwenda mataifa mengine hasa Afrika Kusini.

Chanzo: mwanachidigital