Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wahamiaji haramu 168 watiwa mbaroni Pwani

D1124006e3d3d293e50510055fd1647f Wahamiaji haramu 168 watiwa mbaroni Pwani

Mon, 5 Oct 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

WAHAMIAJI haramu 168 kutoka nchi mbalimbali wamekamatwa mkoani Pwani kwa kuingia nchini kinyume cha sheria.

Naibu Kamishna wa Uhamaji Mkoa wa Pwani, Paulo Eranga aliwaeleza waandishi wa habari ofisini kwake mjini Kibaha jana kuwa wahamiaji hao waliingia nchini kati ya Septemba Mosi hadi 31 mwaka huu.

Alisema walikamatwa kwenye maeneo tofauti mkoani humo.

Eranga alisema nchi inayoongoza kwa kuwa na wahamiaji haramu wengi kati ya waliokamatwa ni Ethiopia.

Alisema, watuhumiwa 128 kati ya waliokamatwa, wanatoka nchini humo. Wengine waliokamatwa ni Warundi 28, raia wa Msumbiji wawili, Wakenya wanne, Mgambia mmoja, Mkongo na Muangola mmoja.

"Moja ya sababu ya wahamiaji haramu kuingia nchini ni hali ngumu ya maisha, raia wa Ethiopia wanafanya nchi yetu kama njia kuelekea kusini mwa Afrika kutafuta maisha na wale wa nchi jirani wanakuja kufanya vibarua ili kujikimu," alisema Eranga.

Alisema changamoto kubwa kwa mkoa wa Pwani ni haina kituo maalumu cha kuingilia wageni, kama ilivyo mpaka wa Namanga. Pia, alisema mkoa wa Pwani una bandari bubu nyingi kwenye mito na bahari.

"Maeneo mengi ya mkoa wa Pwani yana misitu, mapori mengi na uwanda mkubwa wa pwani, maeneo ya bahari kuingia nchi kavu hayafikiki kirahisi, kuna ukosefu wa boti ya doria kwenye bahari na mito, hivyo kufanya urahisi wa kuingia kupitia maeneo hayo," alisema Eranga.

Alisema changamoto nyingine ni baadhi ya wananchi wasio na uzalendo, kushirikiana na mawakala wa wahamiaji haramu kuwaficha na baadhi kuwasafirisha kwa bodaboda wakiwa wamewavalisha nguo za kimasai.

"Pia tunapata ugumu kupata taarifa, kwani kuna watu wanaitwa MINARA ambao huwa wanashirikiana na wasafirishaji hao, kwa kuwapa taarifa kuwa hali ikoje, kama kuna doria ama vipi, ili wahamiaji haramu wafichwe. Hawa taarifa zao tunazo, tunawafuatilia, tutawakamata na kuwachukulia hatua kali za kisheria," alisema Eranga.

Alibainisha ili kudhibiti wahamiaji haramu, inatakiwa ifanywe na watu wote, na si kutegemea vyombo vya usalama peke yake, kwani watu hao hufika kwenye maeneo ya vijiji na mitaa. Hivyo, viongozi wa maeneo hayo, nao wawajibike kwa kutoa taarifa.

"Kuna athari ambazo zinatokana na kuingia kwa wahamiaji haramu, ikiwa ni pamoja na gharama za kuwahifadhi na kuwasafirisha kurudi kwao, ambapo gharama hizi serikali inazipata na kusababisha athari katika uchumi, pia magari yanayokamatwa au nyumba zinazowahifadhi zinataifishwa," alisema Eranga.

Aliongeza wanaendelea kutoa elimu kwa wananchi na kufanya misako kwenye shule,viwanda na kuweka doria maeneo mbalimbali.

Aliwataka wamiliki wa nyumba za wageni, kusajili watu wanaolala kwenye nyumba hizo, ili kudhibiti wahamiaji haramu.

Aliwataka raia wa nje, wanaotaka kuingia nchini, wafuate taratibu ili kuepukana na usumbufu.

Chanzo: habarileo.co.tz