Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wahamiaji haramu 10 wakamatwa wakiwa ndani ya lori la mafuta Songwe

34614 Waamiaji+pic Tanzania Web Photo

Fri, 4 Jan 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mbozi/Morogoro. Huku wahamiaji haramu 10 raia wa Ethiopia wakikamatwa mwishoni mwa mwaka kwenye lori la mafuta, Idara ya Uhamiaji imesema kuanzia Januari hadi Novemba, mwaka jana wahamiaji 12,600 wamekamatwa nchini.

Wahamiaji hao 10 walikamatwa na Jeshi la Polisi mkoani Songwe katika lori la mafuta lililokuwa likiendeshwa na Christopher Kikwete (42), mkazi wa Kibamba jijini Dar es Salaam.

Kukamatwa kwa wahamiaji hao kumekuja zikiwa zimepita siku nne tangu wahamiaji 13 kati ya 26 raia wa nchi hiyo kupatikana wamefariki dunia eneo la Sangasanga kando ya Barabara ya Morogoro - Iringa mkoani Morogoro.

Wakati Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe, Mathias Nyange akieleza hayo, Kamanda wa Uhamiaji mkoani Morogoro, Sophia Muhindi alisema kuanzia Septemba hadi Novemba, mwaka jana wamewakamata wahamiaji 93.

Akizungumza na Mwananchi, Msemaji wa idara hiyo nchini, Ally Mtanda alisema kati ya Januari hadi Desemba 2017 walikamata wahamiaji 15,000 na Januari hadi Novemba, mwaka jana walikamatwa wahamiaji 12,600.

Alisema kati ya waliokamatwa mwaka jana, 6,918 walirudishwa nchini mwao huku 2,499 wakishtakiwa mahakamani.

Mtanda alisema wahamiaji 262 walifungwa, 1,897 kesi zao zinaendelea na 930 upelelezi bado unaendelea.

“Suala la wahamiaji si la Tanzania pekee, ni la dunia nzima na ndio maana Watanzania 1,095 walikamatwa na kurejeshwa nchini na wengi walitokea Msumbiji,” alisema Mtanda.

Alisema jitihada mbalimbali zinafanyika ili kuhakikisha Tanzania haigeuki kuwa ‘uchochoro’ wa kupitisha wahamiaji na kuomba ushirikiano wa wadau na wananchi kufanikisha mapambano hayo.

Awali, katika ufafanuzi wake, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe, Nyange, alisema dereva huyo alikamatwa Desemba 31, mwaka jana katika Stendi ya Mabasi ya Makaburini mjini Vwawa wilayani Mbozi.

Alisema maofisa uhamiaji wakiwa katika doria walilisimamisha lori hilo na kuwakuta wahamiaji hao wakiwa wameketi katika kitanda kilichopo nyuma ya kiti cha dereva.

Aliwataja wahamiaji hao kuwa ni Alemo Hile (21), Debere Sheyiso (17), Mguro Makango (16), Zamade Fikire (17), Beruno Dobmo (14), Belete Mokopo (15), Teruno Dobmo, Eyasu Tefse (15), Abera Abebe (14) na Solomon Abeyin (13).

Kamanda huyo alisema lori hilo lenye namba T 500 DFJ na tela lenye namba T 833CMN aina ya Scania lilikuwa limepakia petroli likitokea Dar es Salaam kwenda nchini Zambia na kwamba, hivi sasa linashikiliwa na polisi.

Kaimu Ofisa Uhamiaji mkoani Songwe, Mariam Mwanzalima alisema dereva wa lori hilo anakabiliwa na mashtaka mawili ikiwamo kusafirisha abiria katika lori na usafirishaji wa wahamiaji haramu.

“Kwa sasa taratibu nyingine za kisheria zinafanyika na iwapo zitakamilika watu hao watafikishwa mahakamani,” alisema Mwanzalima.



Chanzo: mwananchi.co.tz