Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Waganga wa jadi 19 mbaroni kwa kutokuwa na kibali

Mon, 1 Apr 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Shinyanga.  Waganga wa jadi 19 wanashikiliwa na jeshi la polisi mkoani Shinyanga kwa tuhuma za kufanya shughuli za uganga wa jadi bila kuwa na kibali,pamoja na kupiga ramli chonganishi ambazo zimekuwa zikichangia mauaji na wengine kuwekeana chuki.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake leo Jumamosi Machi 30, 2019 kamanda wa Jeshi la Polisi mkoa wa Shinyanga,  Richard Abwao amesema watuhumiwa hao wamekamatwa katika msako uliofanyika kwa siku nne kuanzia March 25, katika wilaya zote za mkoa wa Shinyanga.

Kamanda Abwao alisema  miongoni mwa waganga hao wanawake ni wanne ambao pia watuhumiwa  wamekutwa wana nyara za serikali zinazosadikiwa kuwa ni ngozi na kucha za simba,mayai ya mbuni na pembe za korongo.

Kamanda Abwao alizitaja nyara zingine kuwa ni Ngozi ya nyegere,mikia ya nyumbu, kichwa cha kenge na jino la ngiri ambavyo walikuwa wanavitumia kupigia ramli  chonganishi huku akibainisha kuwa maeneo yaliyokithiri kwa kupiga ramli chonganishi ni Kishapu na Shinyanga vijijini.

“Upigaji wa ramli chonganishi unasababisha madhara makubwa katika jamii kutokana na watu kujengeana chuki na kufikia hatua ya kusababisha mauaji,ninaishauri jamii ibadilike waache kukimbilia kwa waganga wa jadi mtu akiugua aende hospitali kutibiwa”alisema Kamanda Abwao.

Katika msako huo jeshi la polisi liliwakamata watuhumiwa wengine 16 kati yao 9 wakiwa ni wanawake walipatikana wakiwa na madawa ya kulevya,ikiwemo bangi yenye uzito wa kilogramu 35na Heroine gramu 195 ambapo wote watafikishwa mahakamani.

Watuhumiwa wengine saba wote wakiwa ni wanaume wamekamatwa kutokana na kukutwa na mali zinazodhaniwa kuwa ni za wizi zikiwemo friji,Radio Subwoof,baiskeli,pikipiki ,na kingamuzi huku akitumia fursa hiyo kuwataka wananchi kuendelea kutoa ushirikiano.

 



Chanzo: mwananchi.co.tz