Bodi ya Parole Taifa imeridhia wafungwa 49 kunufaika na utaratibu huo baada ya kupokea maombi ya wafungwa 71 kutoka mikoa 16 na kujadiliwa kwa kina kwa mujibu wa sheria na taratibu.
Parole ni mpango wa kumruhusu mfungwa kutoka gerezani na kukamilisha kifungo akiwa uraiani kwa masharti ya kuwa na tabia njema.
Mwenyekiti wa Bodi ya Parole, Balozi Khamis Kagasheki amesema hayo leo Desemba 26,2023 alipozungumza na waandishi wa habari baada ya kufanyika kikao cha 49 cha bodi hiyo mjini Morogoro.
Balozi Kagasheki amesema maombi yao yameanza kujadiliwa ngazi ya mkoa kwa kuyapitia na kuletwa kwenye ngazi ya sekretarieti ya Taifa na kuwasilishwa kwenye Bodi ya Parole Taifa.
“Kikao chetu cha Bodi ya Parole cha 49 kilichofanyika Morogoro ajenda yake kuu ilikuwa kutazama wafungwa walioleta maombi rasmi kupitia ngazi mbalimbali za parole zikiwemo za mikoa,” amesema Balozi Kagasheki.
Amesema wajumbe wa bodi hiyo wamepitia vigezo vyote, hivyo kuona wafungwa 49 wanakidhi vigezo kati 71 waliowasilisha maombi.
Amesema bodi hiyo itawasilisha mapendekezo hayo kwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi ambaye akiridhia watoke gerezani, majina hayo yatateremshwa ngazi za chini ili wahusika wanufaike.
Amewataja wafungwa ambao hawawezi kunufaiki na parole ni wale waliofungwa kwa makosa ya dawa za kulevya, biashara ya kusafirisha binadamu, waliolawiti ama vitendo vya kunajisi.
Kwa upande wake, Kamishna Jenerali wa Magereza (CGP), Mzee Ramadhani Nyamka, amesema sheria ya parole imeweka wazi vigezo vya mfungwa anayelengwa ni yule aliyefungwa kuanzia miaka minne na kuendelea.
Nyamka ambaye ni katibu wa bodi hiyo, amesema sheria inatamka pamoja na kufungwa miaka minne na kundelea, ni lazima awe ametumikia theluthi moja ya kifungo chake na tabia na mwenendo wake uwe wa kuridhika na wakupigiwa mfano na gereza husika.
“Hivi vigezo vinamwezesha mfungwa anaruhusiwa kuomba kwenda kunufaika na mpango wa parole,” amesema Kamishna Jenerali Nyamka.
Amesema kabla ya kufikiwa kwa uamuzi huo, mchakato wa kutafuta maoni unafanyika yakiwemo ya mfungwa mwenyewe alikotoka kijiji, kitongoji au kwenye mtaa.
“Maoni yake mfungwa akieleza alikotoka ile jamii endapo imekubali kumpokea na kushirikiana naye atakaporudi kijijini awe kwenye mazingira ya nyumbani na kuwa na nafasi ya kuihudumia familia yake,” amesema Kamishna Jenerali Nyamka.
Nyamka amesema shughuli zake atazifanyia kijijini hapo ya kumalizika kifungo chake na endapo akiona kwao mazingira si mazuri ana fursa ya kupendekeza eneo lingine atakakoweza kutekeleza sehemu yake ya kifungo chini ya mpango wa parole kwa amani na ufanisi wa hali ya juu.
Amesema kazi ya magereza ni wasimamizi na wafuatiliaji kwenye eneo hilo na kujiridhisha endapo mfungwa yupo sawa na walivyokubaliana akiendelea na shughuli za kawaida alizokuwa akizifanya za kuendesha maisha na kujipatia kipato.
“Akitenda kosa lolote huko kunufaika kwake na mpango wa Parole, utakuwa imefikia tamati na atarudi gerezani na kuendelea kutumikia sehemu iliyobaki ndani ya gereza,” amesisitiza.
Pia amesema kati ya wafungwa 71 waliyokuwa wameomba kwa utaratibu huo wa parole mwanamke alikuwa mmoja, hakukidhi vigezo, hivyo maomba yake yamekataliwa na ataendelea na kifungo.