Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wafanyakazi wa kampuni ya Tigo wahukumiwa kifungo cha nje, warejesha Sh20 milioni

Thu, 17 Oct 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu  Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam nchini Tanzania imewahukumu kifungo cha nje cha miezi sita washtakiwa watano wakiwamo watatu kampuni ya simu ya Tigo waliokuwa wakikabiliwa na mashtaka ya kujipatia fedha  kwa ulaghai ambapo wamerejesha Sh20.3 milioni.

Wafanyakazi hao wa Tigo ni Kokubelwa Karashani na Khalfan Milao ambao ni maofisa huduma kwa wateja kutoka Mliman City na Godfrey Magoye ni wakala wa tigo makao makuu.

Wengine ni  Mohamed Abdallah mkazi wa Kinyerezi na Moses Kilosa ni mkazi wa kibangu.

Washtakiwa hao wamehukumiwa leo Jumatano Oktoba 16, 2019 na Hakimu Mkazi Mwandamizi  Augustine Rwizile  baada ya kukiri kosa hilo.

Akitoa Hukumu hiyo, Hakimu Rwizile amesema amesikiliza hoja za pande mbili na kwamba anawahukumu kutumikia kifungo cha nje cha miezi na kutaifisha sare  moja ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), pingu moja, simu za mkononi 13 pamoja na raini zake  na kuwa mali ya serikali.

Kabla ya kutolewa kwa hukumu hiyo, wakili wa serikali mwandamizi, Awamu Mbagwa amesema hawana kumbukumbu za makosa ya nyuma za washtakiwa hao hivyo ni wakosaji wa mara ya kwanza.

Pia Soma

Advertisement
Mbagwa amedai kufuatia makubaliano ya washtakiwa waliyoingia na Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP ) hawapendekezi kutoa adhabu kubwa hivyo washtakiwa walikubali kulipa Sh20.3 milioni  na zimekwishalipwa.

Pia, ameiomba mahakama itaifishe vielelezo vilivyotumika katika uhalifu huo ambavyo ni simu 13 pamoja na  laini zake, pingu  na sare za JWTZ.

Kwa upande wa utetezi, mshtakiwa Kilosa aliomba isiwape adhabu nyingine kwa kuwa fedha walizolipa  Sh20.3 milioni ni adhabu kubwa kwao na kwamba wanafamilia zinazowategemea .

Hata hivyo, ilibainishwa mahakamani hapo kuwa mshtakiwa  Abdallah na  Kilosa walikuwa marafiki kazi yao ilikuwa ni kuwatapeli watu kwa kutumia ujumbe wa simu za mkononi kwa kushirikiana na wafanyakazi wa Tigo  Karashani na Milao pamoja na Mgoye ni wakala wa Tigo

Awali, washtakiwa hao walikuwa wanakabiliwa na mashtaka sita kati ya hayo yaliyoondolewa ni la utakatishaji wa fedha, kula njama, kupatikana na sare za serikali.

Mahakama hiyo ilielezwa  Januari Mosi 2018 na Juni 20,2019 katika maeneo tofauti kati ya Dar es Salaam na Arusha washtakiwa hao walijipatia Sh20.37 milioni mali ya wateja wa kampuni ya Tigo ambazo walizitoa kutoka Tigo Pesa bila kuwa na kibali chao.

 

Chanzo: mwananchi.co.tz