Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wafanyakazi wa 'Yatch Club' wamburuza mahakamani meneja

Yatch.png Lucy Kimwaga aliyekua mfanyakazi wa Yatch Club akizungumza na waandishi wa habari

Wed, 16 Feb 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wafanyakazi 49 wa Kampuni ya Dar es Salaam Yacht Club wamemfikisha mwajiri wao katika Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA) baada ya kushindwa kufikia muafaka kuhusu mgogoro baina yao na kampuni hiyo.

Mgogoro huo ambao umedumu kwa miaka kadhaa sasa umedaiwa kusababishwa na Meneja wa Kampuni hiyo, Brian Fernandes kwa kushindwa kufuata taratibu za ajira kwa mujibu wa Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini ya mwaka 2004.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana kwa niaba ya wafanyakazi hao, Wakili kutoka Kampuni ya Mawakili ya CS, Claus Thomas Mwainoma amesema tayari wamepata hati ya wito (summons) ambayo imepanga tarehe ya kusikilizwa kwa shauri hilo.

Amesema kwa mujibu wa CMA shauri hilo limepangwa kusikilizwa tarehe 14 Machi mwaka huu.

Amesema hatua hiyo imefikiwa baada ya wafanyakazi hao kuketi na muajiri wao mara kadhaa bila kufikia muafaka.

“Wamekuwa na malumbano baina ya wafanyakazi na mwajiri, wamejaribu kutumia njia mbadala ikiwamo kumuona muajiri kufanya vikao vya ndani na vyama vya wafanyakazi lakini mgogoro huo haukufikia muafaka.

“Wanasema mgogoro umekuwepo kwa muda mrefu, wamejaribu kutafuta suluhu imeshindakana na kwa mujibu wa sheria za kazi, tuliwaelekeza na kuwashauri suala hili lifike kwenye ngazi za kisheria,” amesema.

Aidha, amesema tayari muajiri yaani Brian Fernandes amejulishwa kuhusu suala hilo baada ya kujaza fomu kama sheria inavyotaka.“Tumeshapewa hati ya wito ambayo tutaipeleka kwa muajiri yaani Yacht Club kwa ajili ya kuja kusikiliza malalamiko ya wafanyakazi hao,” amesema.

Aidha, ameyataja malalamiko hayo ya wafanyakazi dhidi ya muajiri wao kuwa ni unyanyasaji wa mahala pa kazi, kunyimwa haki ya kujiunga na vyama vya ushirika na kutokuwepo kwa sera ya Ajira na "scheme of service" pamoja na mpango wa mafunzo.

Pia amesema ndani ya malalamiko ni kwamba kampuni hiyo ya Yacht Club haisimamii kigezo cha fursa sawa kwa watu wote wakati wa kuajiri hali ambayo baadhi ya wafanyakazi hao kumlalamikia meneja huyo anayedaiwa kulipwa mshahara wa zaidi ya Sh milioni 22 kwa mwezi.

“Shauri litasikilishwa ikishindikana tutasonga mbele kutafuta haki. Kwa sababu sheria ya ajira na mahusiano mahala pa kazi ipo kwa ajili ya kulinda haki za mwajiri na haki za mfanyakazi, sheria ipo kwa ajili ya kutetea pande zote,” amesema.

Aidha, mmoja wa wahanga wa madai hayo Lucy Kimwaga ambaye alikuwa mwajiriwa wa Dar es Salaam Yacht Club, amesema malalamiko ya aina hiyo ndiyo yaliyomsababisha kuachishwa kazi kinyemela mwaka 2018.

Amedai licha ya kufanya kazi ndani ya kampuni hiyo kwa muda wa miaka 17 katika nafasi ya afisa manunuzi (Procurement), mwaka 2018 alichishwa kazi baada ya kudaiwa amepokea mzigo wa soda pungufu ulioletwa ndani ya kampuni hiyo.

Amedai alianza kufanyiwa figisu kwa kutolewa kwenye idara manunuzi ambayo ameisomea na kuhamishiwa kuwa katibu mukhtasi (secretary) kisha akapewa barua ya kusimamishwa kazi.

Amedai baada ya kutokea yote hayo, alienda CMA ambako alipata haki kwa kushinda kesi lakini Yacht Club walikata rufaa makahama kuu ambako pia alishinda.

Amedai kampuni hiyo iliagizwa alipwe mishahara yake yote na kurejeshwa kazini lakini kampuni ililipa fidia na kugoma kumrejesha kazini.

“Kiujumla Meneja hataki chama cha wafanyakazi, hurusiwi kuingia kwenye chama cha wafanyakazi, kuna mmoja alijiunga lakini ikawa ni chuki akatolewa kwenye kazi na kuwa kama mtu wa kurandaranda. Baadae waliojiunga sasa wanalaghaiwa watoke ili awe na uwezo wa kuendelea kuwakandamiza,” amedai.

Aidha, kwa mujibu wa katiba ya YACHT Club wafanyakazi hao hawatakiwi kufikisha madai yao kwenye uongozi wa juu (Committee) na badala yake Rais na Makamu wa Rais wa kampuni hiyo wamekasimu madaraka kwa meneja huyo ksuhughulikia mambo yote ya kampuni jambo linalodaiwa kusababisha mgogoro zaidi yao ya wafanyakazi na kampuni.

Akizungumzia madai hayo, Ofisa Rasilimali Watu wa Kampuni hiyo, Esther Kimaro alikiri kufahamu mgogoro huo ambao umefikishwa CMA.

Hata hivyo, hakutaka kufafanua kwa kina madai ya wafanyakazi hao.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live