Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wafanyakazi TPA, CRDB kortini hasara ya bilioni 5/-

E0316defaaea5fd266ba4f2b3577f5cd Wafanyakazi TPA, CRDB kortini hasara ya bilioni 5/-

Thu, 10 Sep 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

WAFANYAKAZI watano wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) na Benki ya CRDB wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam wakikabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi yenye mashitaka 28, likiwemo la kuisababishia TPA hasara ya zaidi ya Sh bilioni 5.1.

Wafanyakazi wa TPA ni Valentine Sangawe (40) ambaye ni mhasibu, na makarani wawili Leticia Massaro (33) na Christina Temu (37), wakati wale wa Benki ya CRDB ni Eva Vicent (33) na Joseph Ndulu. Washitakiwa wote walisomewa mashitaka mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi.

Wakili wa Serikali, Faraji Ngukah alidai washitakiwa hao wanakabiliwa na mashitaka 28, likiwemo la kugushi nyaraka ambazo ni risiti za malipo wakionesha ni halali zilizotolewa katika mfumo wa malipo wa TPA.

Mashitaka mengine ni ya wizi kuisababishia TPA hasara ya Sh 1,119,839,78.28 na kutakatisha Sh 5,119,839,758.28.

Ilidaiwa mahakamani kuwa washitakiwa hao walitenda makosa hayo kati ya Julai mwaka 2014 hadi Aprili mwaka 2015 katika maeneo ya jijini Dar es Salaam, ikiwemo bandari kavu ya TRH.

Ilidaiwa kwamba kati ya Julai 2014 na Mei 2015, maeneo ya bandari kavu ya TRH jijini Dar es Salaam, washitakiwa kwa pamoja walisababishia TPA hasara ya Sh 1,119,839,78.28. Pia alidai kuwa washitakiwa wakiwa watumishi waliiba Sh bilioni 5.1.

Katika mashitaka ya tatu hadi 13, mshitakiwa Sangawe anadaiwa alighushi nyaraka akionesha kuwa Kampuni ya Smart Clearing & Forwarding iliilipa TPA kupitia Benki ya CRDB wakati akijua si kweli.

Katika mashitaka ya 14 hadi 15 ya kughushi ambayo yanamkabili Massaro, Temu wanakabiliwa na mashitaka saba ya kughushi nyaraka mbalimbali. Ngukah alidai Januari 21, 2015 na Januari 22, mwaka huo Vicent aliiba Sh 14,801,238 mali ya TPA.

Pia inadaiwa kati ya Oktoba 30, 2014 na Novemba Mosi 2014, washitakiwa Sangawe, Ndulu na Temu walitengeneza nyaraka za uongo yenye thamani ya Sh 39,992,142.69 kuonesha Kampuni ya Smart imelipa fedha hiyo kwa TPA kupitia Benki ya CRDB wakati si kweli.

Mshitakiwa Ndulu anadaiwa Septemba 29, 2014 na Oktoba 13, 2014 mwaka huo alijipatia Dola za Marekani 8,717.69 mali ya TPA.

Washitakiwa kwa pamoja wanadaiwa walitakatisha Sh bilioni 5.1 wakati wakifahamu kuwa fedha hizo ni zao la kosa la wizi.

Baada ya kusomewa mashitaka hayo, washitakiwa hao hawakutakiwa kujibu lolote kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo. Upande wa mashitaka ulidai upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika na uliomba tarehe nyingine ya kutajwa.

Mshitakiwa Temu alidai kesi hiyo si mgeni, kwani walishitakiwa tangu Desemba mwaka jana na kwamba upelelezi wa kesi hiyo ulianza tangu 2015.

Alidai yeye ni mama ambaye ameacha familia akiwemo mtoto wa mwaka mmoja, na amesimamishwa kazi hivyo hana kipato chochote anachoingiza hali inayosababisha maisha ya watoto wake kuwa magumu.

Hakimu Shaidi aliutaka upande wa mashitaka, kushughulikia malalamiko ya washitakiwa, kwani wao ni binadamu kama wengine na haipendezi kusikiliza malalamiko kila siku.

Baada ya kueleza hayo, Hakimu Shaidi aliahirisha kesi hiyo hadi Septemba 23, mwaka huu itakapotajwa.

Washitakiwa walirudishwa rumande, kwa kuwa mashitaka yanayowakabili hayana dhamana kisheria.

Chanzo: habarileo.co.tz