Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wafanyakazi TBS matatani tuhuma unyang’anyi mil 20/-

Fddbdeab3e7cc0844c5364b50e843257 Wafanyakazi TBS matatani tuhuma unyang’anyi mil 20/-

Wed, 17 Feb 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

NAIBU Waziri wa Viwanda na Biashara, Exaud Kigahe, ameliagiza Shirika la Viwango Tanzania (TBS) liwasimamishe kazi wafanyakazi watatu kwa tuhuma za kufanya unyang'anyi kwa wamiliki wa kiwanda cha Smart kilichopo Kijitonyama, jijini Dar es Salaam wakitaka kulipwa sh. milioni 100.

Kigahe jana pia aliagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kwa kushirikiana na Polisi wafanye uchunguzi dhidi ya maofisa hao.

Alitoa maelekezo hayo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari makao makuu ya TBS, jijini Dar es Salaam.

Aliwataja watumishi hao kuwa ni Ofisa Viwango wa TBS, Sulemain Banza, Ofisa Usafirishaji, Thomas Elisha na dereva, Issa Dodo na watu wengine ambao hakuwataja majina waliojitambulisha kuwa ni Polisi.

Alisema Februali 12 mwaka huu watuhumia hao walienda kwenye kiwanda hicho wakitaka kufanya ukaguzi kwa madai kuwa kinazalisha bidhaa kwa kutumia malighafi zilizoisha muda wake.

Kigahe aAlisema watumishi hao hawakuwa wametumwa na TBS na kwamba Banza aliingilia majukumu ya watu wengine kwenda kufanya ukaguzi, wakati kazi zake ni afisa viwango na si mkaguzi.

Kwa mujibu wa Kigahe ,baada ya kufika kiwandani hapo walitaka walipwe sh. milioni 100 ili waweze kuachana na suala hilo, lakini mwenye kiwanda hakuwa na kiasi hicho cha fedha.

Alisema baada ya hapo walitaka walipwe sh. milioni 50, ambazo nazo mwenye kiwanda hakuwa nazo ndipo walipotaka sh. milioni 20.

Kigahe alisema, mmiliki wa kiwanda hicho aliwaeleza kuwa, kwenye kaunti yake alikuwa na sh. milioni 10 na mke wake sh. milioni 10.

Alisema mmiliki wa kiwanda hicho, mke wake na mhasibu walisindikizwa wakiwa chini ya ulinzi wa watu waliojitambulisha kuwa ni Polisi, huku wakiwa wamenyang'anywa simu zao hadi benki na walipotoa fedha sh. milioni 20 na kuwakabidhi waliwaachia.

Kigahe alisema baada ya kuachiwa mwenye kiwanda na mkewe walipiga simu wizarani na kutoa taarifa kuhusu tukio hilo.

Alisema kitendo hicho ni unyang'anyi wa hali ya juu na hakikubaliki katika kipindi hiki ambacho serikali imetengeneza mazingira kuvutia wawekezaji wajenge viwanda.

"Matukio haya kwa wawekezaji hayawezi kufumbiwa macho na tunalaani tukio hili," alisema Kigahe na kusisitiza kuwa wahusika wa tukio hilo walitumia utashi wao kufanya unyang'anyi, hivyo serikali haiwezi kuwavumilia.

Aliiagiza TBS licha ya kuwasimamisha kazi ichukue hatua nyingine za kinidhamu kwa mujibu wa sheria za kazi.

Chanzo: habarileo.co.tz