Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wafanyabiashara waliotishiana bastora waitwa mahakamani

B62650ade690f8a2f43b449b17009798.jpeg Wafanyabiashara waliotishiana bastora waitwa mahakamani

Sat, 22 May 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

SAKATA la wafanyabiashara wawili, William Taitas Mollel na Dk Philemon Mollel maarufu kwa jina la Monabani wakazi wa jijini la Arusha kutishiana kuuana kwa silaha wakigombea eneo ekari saba lililoamuriwa na Mahakama Kuu, limechukua sura mpya baada ya wafanyabiashara hao kuitwa mahakamani .

Jaji Abdalah Gwae wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, aliwataka wafanyabiashara hao kuacha kuhatarisha amani ya nchi na wazingatie maamuzi yaliyotolewa na mahakama hiyo na si vinginevyo.

Awali, mfanyabiashara Dk Mollel anayewakilishwa na wakili Kapirimpiti Mgalula mahakamani hapo, alilalamika kuondolewa kibabe katika eneo alilowekeza kituo cha mafuta bila kufuata utaratibu baada ya mahakama kudai ni mvamizi.

Mollel aliandika barua ya malalamiko dhidi ya William Titus Mollel na Peter Temu ambao ni wasimamizi wa mirathi ya marehemu Titus Aaron Mollel ambao walishinda Kesi ya Ardhi namba 1 ya Mwaka 2017 dhidi ya Philemon Mollel (Monaban) kumuondoa katika eneo hilo bila kufuata taratibu.

Katika uamuzi uliotolewa Mei 7, mwaka huu na Jaji Mfawidhi wa Mahakama hiyo Kanda ya Arusha, Moses Mzuna, alitamka kwamba Dk Mollel ni mvamizi wa eneo la marehemu Titus Mollel lililoko Ngulelo jijini Arusha na hivyo, kutakiwa kuondoka kwenye eneo hilo lenye ukubwa wa ekeri saba.

Hata hivyo Jaji Gwae, baada ya kusikiliza madai ya pande zote mbili kwa niaba ya Jaji Mfawidhi Moses Mzuna. alifahamisha pande zote kutumia busara na kutohatarisha amani kwa kuwa jambo hilo lilishaamuriwa na Mahakama Kuu.

“Mahakama Kuu imeonelea ni vyema kuita pande zote mbili ili kusisitiza uzingatiwaji wa sheria na utunzwaji wa amani na si kutoa maamuzi mengine yoyote kwa kuwa kesi ilishakwisha kuamuliwa na jalada husika la kesi limefungwa,” alisema Jaji Gwae.

Hata hivyo, wakili Mosses Mahuna aliifahamisha mahakama hiyo kwamba jambo hilo kwa sasa liko polisi baada ya Dk Mollel kuondolewa kwenye eneo na kuleta vurugu zilizosabahisha wafanyabiashara hao kurushiana risasi.

Jaji Gwae alisisitiza kuwa pande zote zizingatie maelekezo yote yatakayotolewa na vyombo vya usalama katika kuhakikisha amani inakuwepo na kulitaka Jeshi la Polisi kuendelea kuimarisha ulinzi katika kituo hicho cha mafuta bila kuingiliwa na pande zote zinazohasimiana.

Chanzo: www.habarileo.co.tz