Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wafanyabiashara waliodhulumu nyumba, viwanja K’koo kukiona

0bf68b930c2ba56e1a3b65d0f3cf9dfd.jpeg Wafanyabiashara waliodhulumu nyumba, viwanja K’koo kukiona

Sun, 17 Jan 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) inakamilisha uchunguzi kwa baadhi ya wafanyabiashara wa Kariakoo jijini Dar es Salaam wanaodaiwa kujipatia viwanja na majumba katika eneo hilo kwa njia ya dhuluma na wengine wakidaiwa kukwepa kodi ya zaidi ya Sh bilioni saba.

Kamanda wa Takukuru wa Mkoa wa Ilala, Christopher Myava alieleza hayo jana wakati akitoa taarifa ya utendaji wa taasisi hiyo kwa kipindi cha robo mwaka kuanzia Oktoba hadi Desemba mwaka jana.

Myava alisema uchunguzi wa matukio hayo na mengine yanayohusu vitendo vya rushwa, utakamilishwa kuanzia mwezi huu hadi Machi mwaka huu.

"Takukuru mkoa wa Ilala imekuwa ikipokea taarifa mbalimbali na kuzifanyia uchunguzi na kuwachukulia hatua wale wanaobainika kutenda kweli makosa hayo, lengo ni kuijenga Tanzania isiyo na rushwa," alisema Myava

Myava alisema pia wanafanya uchunguzi wa zaidi ya Sh bilioni 5.7 za PSSSF zilizokopeshwa kwenye Saccos zilizopo kwenye taasisi mbalimbali za Serikali na taasisi hizo kushindwa kufanya marejesho kwa wakati.

"Mbali na fedha hizo lakini pia katika kipindi hicho, tumeweza kudhibiti upotevu wa fedha kiasi cha Sh Milioni 5.3 kutoka kwa wadaiwa sugu wa vikoba na saccos, na fedha husika kupatiwa kwa sacoss na vikoba husika" aliongeza Myava

Alisema taasisi inaendelea na mashauri 22 yaliyopo mahakamani yakiwamo mapya mawili yaliyofunguliwa hivi karibuni. Miongoni mwa mashauri hayo yanazihusu Mamlaka ya Mapato Tanzania(TRA), Mamlaka ya Maji Safi na Salama Dar es Salaam (Dawasa) Wakala wa Ujenzi wa Barabara (Tanroads) pamoja na Takukuru yenyewe.

Kamanda huyo wa takukuru alisema katika kipindi hicho cha miaka mitatu, imepokea taarifa 247 ambazo kati yake, 68 zinahusu malalamiko ya rushwa yaliyotolewa dhidi ya idara mbalimbali ikiongozwa na serikali za mitaa yenye taarifa 16 ikifuatiwa na mahakama yenye taarifa 12. Taasisi nyingine ambazo uchunguzi unaendelea na idadi ya taarifa kwenye mabano ni Polisi (12), ardhi (7)na elimu (6).

Yaokoa mil 570/- Geita, Tabora

Katika hatua nyingine, katika mikoa ya Geita na Tabora, ndani ya kipindi hicho cha miezi mitatu, Takukuru imeokoa jumla ya takribani Sh milioni 470 katika mikoa ya Geita na Tabora, zimefanyiwa ubadhirifu kwa njia mbalimbali ikiwamo rushwa, dhuluma na utapeli.

Taaarifa juu ya fedha hizo zilitolewa jana kwa nyakati tofauti na wakuu wa Takukuru wa mikoa hiyo ambako mkoani Tabora, zimeokolewa Sh 336.92 katika sekta mbalimbali na Geita ni Sh.milioni 132.5.

Naibu Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Geita, Azza Mtaita alisema kati ya fedha hizo, Sh milioni 11.7 ni ilizorejeshwa kutokana na uchunguzi katika sekta ya elimu na Tamisemi; Sh milioni 10.1 ni za marejesho ya mikopo mbalimbali waliyokuwa wanadaiwa wakopaji na kisha kushindwa kufanya marejesho.

Mtaita alisema Sh milioni 22.7 ni walizokuwa wakidaiwa watuhumiwa baada ya kushindwa kulipa gharama za vifaa vilivyopelekwa kwenye kampuni zao na Sh milioni 5.4 ni zilizookolewa na kurejeshwa kwa mwalimu aliyetapeliwa kwenye biashara ya mtandao ya Q-NET.

Sh milioni nne zilirejeshwa kwa mlalamikaji baada ya kutoa fedha ajengewe nyuma lakini makubaliano hayakutekelezwa.; Sh.milioni 2.5 ni za posho ambazo walimu walitakiwa kulipwa kwa kazi ya kusahihisha mitihani ya darasa la saba lakini haikuwa hivyo; Sh milioni tisa alizodhulumiwa mkopeshaji na mtuhumiwa alishindwa kufanya marejesho.

Kiasi kingine ni Sh.milioni 16 zilirejeshwa kwa wafugaji waliodaiwa kuombwa rushwa; Sh.milioni moja zilirejeshwa kwa wananchi wa Geita baada ya kufanyiwa utapeli na Sh.milioni 1.1 ni za makato ya wafanyakazi ambayo hayakuwasilishwa PSSF.

"Pia tulikamata na kurejesha chupa 1,900 za viuatilifu ambavyo ni dawa aina ya Duduba 450EC zenye thamani ya Sh.milioni 9.5 zilizokuwa zinatoroshwa kwenda Tabora badala ya kugawiwa kwa wakulima wa pamba mkoani hapa,” alisema Mtaita.

Nyingine ni Sh milioni 28.9 zilizookolewa baada ya kutaka kulipwa kwa madiwani wa Halmashauri ya Nyanghwale lakini baada ya Takukuru kujiridhisha na nyaraka ilibaini zilizolipwa ni Sh milioni 3.4 badala ya Sh milioni 32.3 kama walivyoainisha.

Alieleza, fedha ya Sh.milioni 14.9 ni fedha za mishahara ambazo walikuwa wamedhulumiwa wafanyakazi 20 wa kampuni ya Majaliwa Investment Co.Ltd kama makato ya NSSF lakini mwajiri huyo hakuwahi kuwasilisha fedha hizo.

Kwa upande wa mkoa wa Tabora, Kaimu Mkuu wa Takukuru, Mashauri Elisante alisema Sh milioni 336.92 ziliokolewa kutoka kwenye Amcos , saccos, mapato ya ndani ya halmashauri ,mikopo umiza na watumishi wa muda vibarua kudhulumiwa stahiki zao.

Chanzo: habarileo.co.tz